Tiketi za ndege za kukimbia Israel zawa adimu
(last modified Sun, 01 Jun 2025 10:09:36 GMT )
Jun 01, 2025 10:09 UTC
  • Tiketi za ndege za kukimbia Israel zawa adimu

Soko la usafiri wa anga kutoka maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni limekumbwa na mgogoro usio na kifani kutokana na kuendelea mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya jeshi la Yemen dhidi ya miundombinu muhimu ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa gazeti la Kizayuni la Maariv, mashambulizi ya mara kwa mara ya jeshi la Yemen katika maeneo nyeti na muhimu mno ya utawala wa Kizayuni hususan Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv yamezusha hofu na wasiwasi mkubwa miongoni mwa mashirika ya ndege ya kimataifa na kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama za tiketi za ndege kwenda au kupitia Israel.

Katika toleo lake la karibuni zaidi, gazeti hilo limeripoti kuwa, mwanzoni mwa majira ya joto ya 2025 na kuendelea wimbi la mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Yemen, bei ya tiketi za ndege kutoka Israel imeongezeka kwa kiasi kikubwa, na masharti ya uuzaji tiketi pia yameongeza gharama za usafiri.

Gazeti hilo limeandika: Masharti mazito yaliyowekwa katika ununuzi wa tiketi za ndege yamesababisha shinikizo kubwa la kiuchumi kwa abiria wa kawaida, wakati maafisa wa Israel ambao wanasafiri kwa kutumia madaraja ya juu wanapewa nafasi zaidi kuliko watu wengine na hawahisi sana machungu ya mgogoro huo.

Kabla ya hapo shirika la habari la Saba la Yemen lilikuwa limetangaza jana Jumamosi likimnukuu afisa mmoja wa Yemen akisema kwamba, wawekezaji na makampuni yote ya kigeni yanayofanya kazi Israel yanatahadharishwa kuondoka katika maeneo hayo haraka iwezekanavyo, kwa sababu Israel haitakuwa salama tena na sasa ni wakati mzuri wa kuondoka, kabla ya fursa hiyo kupotea.