Kwa nini Marekani inafuatilia sana kupanua uhusiano na utawala wa Julani?
(last modified Sun, 01 Jun 2025 02:27:21 GMT )
Jun 01, 2025 02:27 UTC
  • Kwa nini Marekani inafuatilia sana kupanua uhusiano na utawala wa Julani?

Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuamuru kuondolewa vikwazo dhidi ya Syria, makazi ya balozi wa Marekani mjini Damascus sasa yamefunguliwa tena baada ya miaka 13.

Mbali na Thomas Barrack, mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani katika masuala ya Syria na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Asaad Al-Shaibani, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya mpito ya Syria pia alihudhuria sherehe za ufunguzi wa makazi hayo ya balozi wa Marekani mjini Damascus. Katika safari hii, Thomas Barak amekutana na Muhammed Julani, mkuu wa serikali ya mpito ya Syria. Wakati wa sherehe za ufunguzi wa makazi hayo, bendera ya Marekani ilipepea juu ya viwanja vya makazi; kitendo ambacho wachambuzi wa mambo wanakichukulia kuwa kielelezo cha hamu ya pande mbili ya kufungua ukurasa mpya katika mahusiano ya nchi mbili.

Aidha, makubaliano yalitiwa saini kati ya makampuni ya Marekani, Qatar na Uturuki kwa lengo la kukarabati gridi ya umeme ya Syria. Matukio haya yanakuja baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuamua kuitambua rasmi serikali mpya ya Syria na kutangaza kuwa ameondoa vikwazo vya miongo kadhaa vya Marekani dhidi ya nchi hiyo ili kusaidia kuimarisha uchumi wake. Kwa hiyo, swali muhimu ni kuwa je, kwa nini Marekani imeweka kupanua uhusiano na serikali ya mpito ya Syria kwenye vipaumbele vya ajenda yake?

Julani

Ili kujibu swali hili, ifahamike kwanza kwamba sababu muhimu zaidi iliyopelekea Marekani kufunga ubalozi wake huko Damascus mwaka 2011 inahusiana na serikali ya zamani ya Damascus. Serikali hiyo, ikiongozwa na Bashar al-Assad, ilipinga vikali kufanya mapatano ya udhalilishaji na utawala wa Kizayuni, na kuamua kushirikiana na mhimili wa muqawama wa eneo la Asia Magharibi unaopinga ubeberu na unyanyasaji wa madola ya Magharibi na vibaraka wao katika eneo. Kwa hiyo, serikali ya Bashar al-Assad nchini Syria ililazimishwa kupigana vita vikali ambavyo havijawahi kushuhudiwa tena tokea 2011, ambapo jeshi la nchi hiyo lililazimika kupambana na makundi ya kigaidi ambayo wanachama wake walitoka zaidi ya nchi 80 duniani. Aidha, Marekani iliiwekea nchi hiyo vikwazo vikali ambavyo vilikuwa na madhara makubwa kwa uchumi wake.

Kufuatia kuanguka kwa utawala wa al-Assad nchini Syria mwezi Disemba mwaka jana, serikali ya Marekani imekuwa ikiona kuimarika kwa serikali nchini Syria ambayo sio tu kwamba haina uwezo wa kujilinda dhidi ya utawala wa Kizayuni, bali pia haina maingiliano yoyote na mhimili wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi. Zaidi ya hayo, serikali ya mpito ya Junali si tishio lolote kwa Marekani na wala haipingi kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na wanajeshi wa Marekani. Kwa hiyo, kufuatia matukio ya hivi karibuni ya kisiasa nchini Syria na kuanguka kwa serikali iliyopita, dalili zimejitokeza za Washington kutaka kufufua uhusiano wake na utawala mpya wa Damascus.

Mwishoni mwa Disemba 2024, chini ya wiki mbili baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad, ujumbe wa kidiplomasia kutoka Marekani ulisafiri hadi Damascus na kufanya mazungumzo na Julani, mkuu wa utawala mpya wa Syria. Kufuatia mkutano huo, serikali ya Marekani iliondoa baadhi ya vikwazo dhidi ya Syria, na katika wiki za hivi karibuni, Donald Trump alikutana na Julani alipokuwa safarini mjini Riyadh Saudi Arabia, ambapo alitangaza rasmi kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Syria. Ijapokuwa hatua ya Marekani ya kuondoa vikwazo na kufungua tena makazi ya balozi wake mjini Damascus inaweza kuimarisha nafasi ya Julani ndani ya Syria, lakini pia inaashiria kwamba Marekani iko tayari hata kushirikiana na magaidi wa zamani na wavaaji suti wa leo kwa ajili tu ya kufuatilia maslahi yake haramu katika eneo. Kauli mbiu ya kupambana na ugaidi kwa mtazamo wa Washington inaweza pia kumaanisha ushirikiano na ugaidi pale maslahi ya Marekani yanapohitaji kulindwa.