Je, Hamas inasisitiza vipaumbele vipi kabla ya kukubali usitishaji mapigano?
(last modified Sun, 01 Jun 2025 06:04:07 GMT )
Jun 01, 2025 06:04 UTC
  • Je, Hamas inasisitiza vipaumbele vipi kabla ya kukubali usitishaji mapigano?

Jihad Taha, Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema: "Tumemuomba mpatanishi wa Marekani atoe dhamana nzito na za kimaandishi kwa ajili ya kusimamisha vita vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza."

Msemaji huyo wa Hamas ameongeza kuwa, harakati hiyo kwa kuwajibika ipaswavyo na kwa uratibu na makundi mengine ya muqawama, imechunguza kwa kina pendekezo lililowasilishwa na mjumbe wa Marekani katika masuala ya Mashariki ya Kati Steve Witkoff kwa ajili ya kusitishwa mapigano Gaza.

Jihad Taha amesema kwamba mpango uliopendekezwa na Witkoff hauna dhamana muhimu, na kwamba hauzingatii matakwa mengi yaliyowasilishwa na Hamas kwa wapatanishi na wala hauna dhamana za wazi.

Msemaji huyo wa Hamas amesisitiza kuwa makubaliano yoyote lazima yajumuishe usitishaji vita kamili na uondokaji kamili wa vikosi vya Israel vinavyokalia kwa mabavu Gaza.

Taha amedokeza kwamba toleo la mwisho la mpango wa Witkoff halina dhamana yoyote ya mara moja au hata ya hatua kwa hatua kwa ajili ya kusitisha vita, na kuongeza: "Tuna shaka kubwa kutokana na mpango wa Witkoff  kuwa na utata mwingi na kutokuwa na dhamana ya wazi."  Msemaji wa Hamas ametoa wito kwa taasisi za kimataifa kutangaza hali ya hatari ili kuinusuru Gaza kutokana na maafa ya kibinadamu.

Awali Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ilitoa taarifa ikisema kwamba inashauriana na pande na makundi ya Palestina kuhusu pendekezo ililopokea hivi karibuni kutoka kwa Steve Witkoff kupitia wapatanishi, mjumbe maalum wa Rais Donald Trump wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, kuhusu usitishaji vita huko Gaza.

Jihad Taha, Msemaji wa Hamas

Hamas imeongeza kuwa imechunguza pendekezo hilo kwa uwajibikaji na kwa njia ambayo inahudumia maslahi ya watu wa Palestina, kudhamini faraja yao na kupelekea kupatikana usitishaji vita wa kudumu huko Gaza.

Viongozi wa Hamas wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba, mipango inayowasilishwa na nchi za Magharibi hususan Wamarekani haishughulikii kusimamisha vita, bali ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni na dhidi ya Wapalestina.

Harakati ya Hamas daima imekuwa ikisisitiza kwamba mipango inayopendekezwa kama vile mpango wa Witkoff kupitia wapatanishi haitoi hakikisho linalohitajika kwa ajili ya kukomesha kukaliwa kwa mabavu Gaza, kurejea kwa wakimbizi wa Kipalestina wala kuasisiwa taifa huru la Palestina lenye mipaka inayotambulika kimataifa.

Mipango hiyo inawasilishwa katika hali ambayo utawala wa Kizayuni unaendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kufanya jinai, yakiwemo mauaji ya raia yanayoendelea sasa huko Gaza.

Hamas na makundi mengine ya mapambano yanapigania ukombozi kamili wa Palestina, wakati mipango mingi iliyowasilishwa na nchi za Magharibi inafuatilia tu masuluhisho yasiyo na faida yoyote kwa Wapalestina, ukiwemo ule wa eti kuasisiwa mataifa mawili ya Wapalestina na Wazayuni.

Kwa hiyo, Hamas haitauamini mpango wowote unaowasilishwa na Wamagharibi hadi pale utakapodhamini maslahi na haki za Wapalestina wote.

Witkoff amewasilisha mpango mpya wa usitishaji vita wa siku 60 na kubadilishana mateka wa Kizayuni, katika hali ambayo mpango huu, sawa na mipango mingine ya awali iliyowasilishwa na utawala wa Kizayuni na washirika wake kuhusu kukaliwa kwa mabavu Ukanda wa Gaza, unaunga mkono kuendelea kuwepo kwa wavamizi katika ukanda huo.

Mielekeo ya upendeleo ya viongozi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni ndio kikwazo kikuu cha kufikiwa makubaliano yoyote ya kuhitimisha vita vya Gaza, na Wazayuni kwa kutumia vibaya fursa hiyo wanaendeleza jinai na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina bila huruma.

Katika hali hiyo, Hamas imesisitiza wazi kwamba usitishaji vita utaanza pale matakwa halali ya Wapalestina yatakapotekelezwa. Kusimamishwa mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Gaza na kuondoa askari wake vamizi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni miongoni mwa masharti makuu ya Hamas ya kukubali usitishaji vita. Makundi mbalimbali ya Palestina yakiwemo ya muqawama yanaunga mkono rasmi misimamo ya Hamas katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni.

Mpango huo mpya wa Witkoff unakuja wakati ambapo jeshi la Israel limeshindwa na kukata tamaa katika kukabiliana na makundi ya wapiganaji wa Palestina.