Iran yatumia nishati ya nyuklia kuzalisha mpunga wakati wa ukame
Uzalishaji wa mpunga aina ya "Kian" ni mafanikio mapya ya matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia nchini Iran. Mpunga huo unastahamili ukame usio na kifani na hilo ni suluhisho la kisayansi la kukabiliana na tatizo la maji katika mashamba ya mpunga.
Shirika la Habari la Tasnim limeandika makala maalumu kuhusu suala hilo na limeandika: "Wakati linapozungumziwa suala la nishati ya nyuklia, akili za watu wengi huenda haraka kwenye uzalishaji wa silaha za maangamizi ya umati, urutubishaji kwa wingi wa madini ya urani au utengezaji mabomu ya atomiki, lakini ukweli ni kuwa, teknolojia ya nyuklia duniani leo imeendea mbali zaidi.
Teknolojia ya nyuklia ina jukumu muhimu katika maendeleo endelevu ya nchi, kuanzia kwenye kuongeza tija ya kilimo hadi kutibu magonjwa yasiyotibika; kutoka kwenye kudhibiti wadudu bila ya kutumia viuatilifu na sumu kali hadi kuboresha usalama wa chakula, yote hayo ni mafanikio yanayoonekana ya sayansi hii tata lakini yenye manufaa makubwa.
Nchini Iran, Shirika la Nishati ya Atomiki pia limekuwa likifanya jitihada kubwa za kustafidi na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani ikiwa ni pamoja na kubuni mbinu sahihi na bora za kustawisha maisha ya kila siku ya watu. Ripoti nyingi juu ya matumizi ya mionzi, uzalishaji wa dawa, mbegu zinazostahamili mazingira magumu sana na teknolojia za uchunguzi katika tasnia ya maziwa ni sehemu ya matunda ya jitihada hizo za kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya kiraia.
Kwa mujibu wa makala hiyo ya Shirika la Habari la Kimataifa la Tasnim, uzalishaji wa aina ya mchele unaoitwa "Kian" ambao unastahamili ukame na ukata wa maji; kupitia Wizara ya Jihad ya Kilimo ya Iran, ni mafanikio mengine makubwa ya kutumiwa vizuri nishati ya nyuklia nchini Iran.