Brigedi za Shahid Muhammad Deif zaanzishwa rasmi Palestina
Brigedi za Shahid Muhammad Deif zimetangaza kuanzishwa rasmi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni sambamba na kutangaza utiifu wake kwa damu toharifu ya mashahidi iliyomwagwa kwenye njia takatifu ya Muqawama na ukombozi wa Palestina.
Brigedi za Shahid Muhammad Deif zimetoa taarifa na kusema: "Sambamba na kutangaza utiifu wetu kwa damu toharifu ya mashahidi wa njia ya Haki na kula kiapo chetu cha kuendeleza njia ya Muqawama, leo (Jumamosi) tunatangaza kuanzishwa Brigedi za Shahid Muhammad Deif katika ardhi za Palestina zinayokaliwa kwa mabavu (na Wazayuni)."
Taarifa hiyo imesema: "Sisi ni kizazi ambacho kilizaliwa chini ya mashambulizi ya mabomu na sauti za bunduki na hatukubali maisha ya kudhalilishwa. Imma tutaishi maisha yanayowafurahisha marafiki au tutakufa shahidi kwa kifo kinachomkasirisha adui."

Taarifa imesema: "Tunamwambia adui Mzayuni kwamba tutakuwa upanga mkali juu ya wanajeshi wako. Popote utakapoangalia utatuona. Tutapigana nawe kwa njia na mbinu zote zitakazowezekana. Tutazitia hofu na kihoro nyoyo zenu na tutakutimueni katika nchi yetu ya Palestina."
Taarifa hiyo inaongeza: "Brigedi za Shahid Muhammad Deif si chama au shirika. Bali ni harakati ya kimapinduzi na huru ambayo imejibanza katika kila uchochoro na barabara na imo katika kila kambi. Sisi ni sauti ya kilio kutoka chini ya kifusi. Sisi ni sauti moja kutoka Ghaza hadi Ukingo wa Magharibi hadi Baytul Muqaddas na hadi katika ardhi zote za Palestina mnazozikalia kwa mabavu. Hatutanyamaza tena. Uwanja wa mapambano ndipo nyumbani petu. Imma ni Jihadi au kufa shahidi!"
Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Alam, shahid "Muhammad Deif", ambaye jina lake halisi ni "Muhammad Diab Ibrahim Al-Masri," aliyepewa lakabu ya "Abu Khaled," alizaliwa mwaka 1965 katika kambi ya wakimbizi ya Khan Yunis kusini mwa Ghaza. Alikuwa kamanda mkuu wa Brigedi za Qassam, tawi la kijeshi la Hamas. Aliuawa shahidi wakati wa vita vya hivi karibuni huko Gaza pamoja na makamanda wengine kadhaa wa brigedi hizo.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaamini kuwa yeye ndiye mpangaji mkuu wa shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba, linalojulikana kwa jina la Kimbunga cha Al-Aqsa.