Israel yamjibu Macron: Kutambuliwa Palestina kutasalia kwenye karatasi tu
(last modified Sat, 31 May 2025 02:22:50 GMT )
May 31, 2025 02:22 UTC
  • Israel yamjibu Macron: Kutambuliwa Palestina kutasalia kwenye karatasi tu

Waziri wa Vita wa Israel, Israel Katz amemsuta na kumkejeli Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye alisema mapema jana kwamba, kutambuliwa kwa taifa la Palestina, kwa masharti, ni "wajibu wa kimaadili."

Katika ziara yake katika Ukingo wa Magharibi jana Ijumaa, Katz alimkemea Macron akisema kwamba "Kutambuliwa kwa taifa la Palestina 'kwenye karatasi' kutakabiliwa na ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni 'kwenye ardhi.'

Ziara ya Katz katika Ukingo wa Magharibi inakuja baada ya Israel kuidhinisha ujenzi wa makazi mapya 22 katika eneo hilo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na ujenzi mpya wa Sa-Nur, ambayo ilihamwa mwaka 2005, sambamba na kujitenga Israel kutoka Ukanda wa Gaza.

Huku akipongeza uamuzi huo wa Tel Aviv na kuitaja kama "lahadha ya kihistoria" kwa walowezi, Katz alisema ujenzi huo unatuma "ujumbe wa wazi kwa Macron na marafiki zake."

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesisitiza haja ya kutambuliwa rasmi Palestina kama taifa. Wakati wa ziara yake nchini Singapore jana (Ijumaa), Macron aliwataka Wazungu kuchukua msimamo wa pamoja dhidi ya Israel na kuainisha masharti ya kuitambua Palestina.

Hata hivyo, Waziri wa Vita wa Israel anasisitiza kuwa, "Watalitambua taifa la Palestina kwenye karatasi - na sisi tutajenga taifa la Kiyahudi la Israel ardhini. Karatasi hiyo itatupwa kwenye jaa la taka za historia, lakini taifa la Israel litaendelea kustawi na kustawi."