Trump amfanyia istihzai Macron kwa kuzabwa kibao na mkewe hadharani+VIDEO
Rais wa Marekani, Donald Trump ameonekana kumfanyia dhihaka mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye hivi karibuni alidhalilishwa na mkewe hadharani.
Wakati waandishi wa habari walipomtaka Trump atoe maoni yake kuhusu tukio la hivi majuzi la Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kuzabwa kibao na mkewe Brigitte machoni pa ulimwengu, rais huyo wa Marekani ametoa matamshi ambayo baadhi ya wadadisi wa mambo wanasema ni ya istihzai.
Waandishi wa habari walipomtaka atoe 'ushauri kidogo' kama "kiongozi wa ulimwengu kwa kiongozi wa ulimwengu" juu ya tukio hilo, Trump alisema, "Hakikisha mlango unabaki umefungwa."
Trump, 78, alitoa matamshi hayo ya kejeli huku akitabasamu kwa dharau, katika mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval, Ikulu ya White House Ijumaa ya jana (Mei 30), akiashiria jinsi tukio hilo la 'faragha' lilivyofanyika mbele ya kamera za waandishi wa habari.
Baada ya dhihaka hiyo, Trump alizungumzia tukio hilo kwa umakini zaidi, akibainisha kuwa, "Nilizungumza naye (Macron) na yuko sawa, wako sawa."
Video inayoonesha mke wa Macron akimzaba kibao mumewe na baadaye kukataa kumshika mkono wakati wanashuka ndege, imeenea kwa kasi ya umeme mitandaoni. Video hiyo iliyoenea sana kwenye mitandao ya kijamii inamuonesha mke wa rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron,Brigitte Marie-Claude Macron ambaye ni bikizee wa miaka 72, akimpiga kibao cha uso mumewe baada ya ndege yao kutua Vietnam.
Ikulu ya Ufaransa Elysee imefanya juhudi za kufifiliza tukio hilo bila ya mafanikio. Ndoa ya Macron imekuwa ya utata tangu mwanzoni, kwani Brigitte wakati huo alikuwa mwalimu wa michezo ya kuigiza aliyekuwa na umri wa miaka 39 katika shule ya Kikatoliki kaskazini mwa Ufaransa alikokuwa akisoma Macron, wakati wakati huo akiwa na umri wa miaka 15, walipoanza kuchumbiana. Awali wazazi wa Macron, hawakuunga mkono uchumba wa wawili hao kutokana na mwanya mkubwa wa umri baina yao.