Wanajeshi kadhaa Nigeria wauawa katika hujuma ya magaidi wa Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126350-wanajeshi_kadhaa_nigeria_wauawa_katika_hujuma_ya_magaidi_wa_boko_haram
Kundi la kigaidi la Boko Haram limevamia kambi ya kijeshi katika eneo la Serikali ya Mitaa ya Marte, Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kuwaua wanajeshi kadhaa.
(last modified 2025-05-13T08:52:50+00:00 )
May 13, 2025 08:52 UTC
  • Wanajeshi kadhaa Nigeria wauawa katika hujuma ya magaidi wa Boko Haram

Kundi la kigaidi la Boko Haram limevamia kambi ya kijeshi katika eneo la Serikali ya Mitaa ya Marte, Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kuwaua wanajeshi kadhaa.

Vyanzo vya kijeshi vinasema kuwa shambulio hilo lilitokea katika Kambi ya Mbele ya Kikosi cha 153 cha Kazi maalum, alfajiri siku ya Jumatatu.

Maafisa waandamizi wa jeshi wamesema kuwa zaidi ya wanajeshi 10 waliuawa katika shambulio hilo.

Walioshuhudia wanasema magaidi walitwaa Marte mapema alfajiri. Zaidi ya wanajeshi 10 waliuawa na mamia ya wengine walikimbia. Aidha magaidi waliteketeza magari ya kivita na kuiba silaha na risasi.

Maafisa wa jeshi la Nigeria bado hawajatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo. Msemaji wa jeshi la Nigeria, Onyechi Anele, amesema uchunguzi bado unaendelea wakati taarifa hii ilipotolewa.

Hili ni shambulio la pili dhidi ya kambi ya kijeshi katika jimbo la Borno, ngome kuu ya Boko Haram, ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Boko Haram, ambalo limekuwa likiendesha hujuma za kigaidi nchini Nigeria tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, limehusika na mashambulizi ya kigaidi ya kutisha tangu mwaka 2009, na kupelekea maelfu kupoteza maisha.