Angola imempa hifadhi Rais wa zamani wa Gabon Ali Bongo aliyefukuzwa madarakani
Rais wa zamani wa Gabon Ali Bongo na familia yake wameachiwa kutoka kizuizi cha nyumbani na kuhamishiwa Angola. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ijumaa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Joao Lourenco.
Hatua hii imetangazwa siku chache baada ya Lourenco, ambaye pia ni rais wa Angola, kutembelea nchi hiyo ya Afrika ya Kati na kufanya mazungumzo na kiongozi wake, Brice Oligui Nguema, aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti 2023 ambayo yalimuondoa Bongo madarakani.
Mke wa Bongo, Sylvia Bongo Ondimba, na mwanawe, Noureddin Bongo Valentin, walihamishwa kutoka gerezani kwenda kizuizini nyumbani wiki iliyopita, baada ya kufungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa tuhuma za ufisadi, rushwa, na utakatishaji fedha. Walihamishiwa makazi ya familia mjini Libreville, mji mkuu wa Gabon.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti awali kuwa mke wa rais huyo wa zamani na mwanawe walikuwa chini ya usimamizi wa kisheria na walitakiwa kushirikiana na mamlaka za ndani wakati kesi yao ikiendelea. Sylvia Bongo alikamatwa rasmi mwezi Oktoba 2023, miezi baada ya mapinduzi. Wakili wake awali alisema kukamatwa kwake kulitokana na sababu za “kibinafsi” na “haramu.”
Familia ya Bongo ilitawala siasa za Gabon kwa zaidi ya miongo mitano. Ali Bongo alichukua madaraka mwaka 2009 kufuatia kifo cha baba yake, Omar Bongo, aliyeongoza tangu mwaka 1967. Urais wa Ali Bongo ulimalizika mwezi Agosti 2023 wakati Jenerali Nguema aliongoza mapinduzi ya kijeshi baada ya uchaguzi wa utata.
Mamlaka za serikali zilimshtaki Sylvia Bongo kwa kutumia vibaya hali duni ya afya ya mumewe , iliyosababishwa na kiharusi cha mwaka 2018, na kupora fedha za umma kwa usaidizi wa maafisa wakuu. Yeye na mwanawe wamekanusha kuhusika na uporoaji huo
Rais huyo wa zamani alifanya mgomo wa kula mwaka jana kama ishara ya kulalamika kuhusu unyanyasaji unaodaiwa kufanywa kwa familia yake wakati walipokuwa mahabusu.
Tarehe 30 Aprili, Umoja wa Afrika uliipitisha azimio la kuitaka serikali kuachilia huru Bongo na familia yake, na kuhimiza uongozi mpya wa zamani koloni la Ufaransa kuzingatia haki zao na usalama wao.
Serikali ya Gabon haijatoa tamko rasmi kuhusu kile ambacho jarida la Gabon Review lililitaja kama kuachiliwa na kuhamishwa kwa familia ya Bongo kwa siri kwenda Angola jirani. Rais Brice Oligui Nguema , aliyeshinda uchaguzi uliopita mwezi uliopita kwa asilimia 90.35 ya kura , pia ni binamu wa Ali Bongo.