Maandamano yazuka mjini Tripoli nchini Libya, mawaziri kadhaa wajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126486-maandamano_yazuka_mjini_tripoli_nchini_libya_mawaziri_kadhaa_wajiuzulu
Maandamano makubwa dhidi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) yalizuka jana Ijumaa mjini Tripoli Libya huku mawaziri kadhaa wakitangaza kujiuzulu.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 16, 2025 23:21 UTC
  • Maandamano yazuka mjini Tripoli nchini Libya, mawaziri kadhaa wajiuzulu

Maandamano makubwa dhidi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) yalizuka jana Ijumaa mjini Tripoli Libya huku mawaziri kadhaa wakitangaza kujiuzulu.

Televisheni ya ndani ya Alwasat imeripoti kwamba waandamanaji wameitaka serikali ya GNU inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdul-Hamid Dbeibah kuondoka madarakani, kufuatia mapigano makali ya hivi karibuni ya mjini Tripoli. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maafisa wakuu wa GNU akiwemo naibu waziri mkuu na mawaziri wa serikali za mitaa, biashara na viwanda, elimu ya juu, nyumba na rasilimali za maji wametangaza rasmi kujiuzulu. Lakini GNU imekanusha kujiuzulu, ikisema maafisa wakuu wote wa serikali "wanafanya kazi zao kama kawaida." GNU imetoa mwito wa maandamano ya amani na kwa uhuru kamili ndani ya mifumo ya kisheria na kwa kulinda taasisi za serikali." 

Mapigano yalizuka mapema wiki hii baada ya Abdel Ghani al-Kikli, anayejulikana pia kwa jina la Ghaniwa, kamanda mkuu wa kundi la SSA ambalo ni kundi lenye nguvu lenye silaha linaloshirikiana na Baraza la Uongozi kuuawa katika kituo kinachodhibitiwa na Brigedi ya 444 ya watiifu kwa Dbeibah. Vyanzo vya usalama vinasema mauaji hayo yalisababisha mapigano makali ya kulipiza kisasi kati ya SSA na Brigedi ya 444 na kuenea katika wilaya za kati na kwenye makazi ya raia na kupelekea watu wasiopungua sita kuuawa. Mapigano hayo yalisitishwa siku ya Jumatano. 

Libya haijawahi kuwa na utulivu wa kudumu tangu ulipotokea uasi wa wananchi mwaka 2011 uliomuondoa madarakari kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi kwa msaada wa jeshi la nchi za Magharibi NATO ambalo lilifanya mashambulizi mabaya ya kuangamiza miundombinu ya Libya na baadaye kuitelekeza nchi hiyo huku silaha zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi hasimu.