Wanasheria wa Kenya wakiongozwa na Karua wazuiwa kuingia Tanzania
Mwanasiasa maarufu wa Kenya Martha Karua ambaye pia ni mwanasheria anayewakilisha vigogo wa upinzani wanaokabiliwa na kesi katika mataifa jirani, amekamatwa nchini Tanzania katika uwanja wa ndege.
Karua amekuwa akimuwakilisha kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini, na anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu.
Msemaji wa Karua amesema mwanasheria huyo alizuiliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa tatu. Pasipoti yake ilichukuliwa na alikuwa akisubiri kurudishwa Kenya.
Waziri huyo wa zamani wa sheria na aliyewahi kuwania urais nchini Kenya, amekuwa mstari wa mbele kupinga kile anachosema ni "kurudishwa nyuma kwa demokrasia" katika eneo la Afrika Mashariki. Pia amekuwa akimuwakilisha kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye, ambaye alitekwa nyara nchini Kenya mwaka jana na kurudishwa nchini kwao pia akikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Uganda itafanya uchaguzi mkuu Januari mwaka ujao.
Martha Karua amethibitisha kuzuiliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, akiwa pamoja na wakili wa masuala ya haki za binadamu kutoka kenya, Lynn Ngugi na mwanachama wa chama cha wanasheria wa Afrika Mashariki, Gloria Kimani.
Kwa mujibu wa maelezo yao, baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dar Es Salaam, pasi zao za kusafiria zilichukuliwa na maofisa wa idara ya usalama, kabla ya baadae kutaarifiwa kuwa hawaruhusiwi kuingia Tanzania, bila hata idara ya uhamiaji kutoa sababu za kuwazuia.