Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Sudan
Umoja wa Mataifa jana Alkhamisi ulionya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayozidi kuwa kali katika nchi ya Sudan iliyoharibiwa vibaya na vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi.
"Ongezeko la mapigano katika maeneo mbalimbali nchini Sudan linawalazimisha raia kutoka katika makazi yao na kukimbilia sehemu nyingine" amesema Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres. "Katika jimbo la Kordofan Magharibi, ukosefu wa usalama umewalazimisha karibu watu 47,000 kutoka katika miji ya Khiwai na Nuhud mwezi huu na kukimbilia sehemu nyingine," amesema msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa, akinukuu Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.
"Wengi wa watu hawa tayari walikuwa wakimbizi wa ndani na sasa wanalazimika kuhama kwa mara ya pili," amesema. "Katika jimbo la Darfur Kaskazini, takriban watu 1,000 wamekimbia makazi yao kutoka kambi ya Abu Shouk na mji wa El Fasher katika wiki moja iliyopita, na kufanya jumla ya watu waliokimbia makazi yao kutoka maeneo hayo mawili mwezi huu kufikia 6,000. Kwa ujumla, Darfur Kaskazini inakadiriwa kupokea zaidi ya watu milioni 1.7 waliokimbia makazi yao," amesema.
Aidha Stephane Dujarric amesema: "Kupanda bei ya vyakula kunazidisha mgogoro. Umoja wa Mataifa pia unasikitishwa na kuongezeka kesi za ugonjwa wa kipindupindu katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Khartoum. "Hali mbaya ya mji mkuu wa Khartoum inachangiwa na kukatika umeme katika kipindi cha wiki moja iliyopita, ikiripotiwa kusababishwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye miundombinu muhimu ya umeme. Hii imetatiza sana upatikanaji wa maji na huduma za afya. Watu wanakimbilia vyanzo vya maji visivyo salama, jambo ambalo linaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa yatokanayo na maji," amesema.