Rais wa Zambia atoa wito wa mshikamano na amani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126838-rais_wa_zambia_atoa_wito_wa_mshikamano_na_amani_afrika
Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, siku ya Jumapili alitoa wito wa mshikamano wa Kiafrika na maendeleo jumuishi wakati bara la Afrika likiadhimisha miaka 62 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 26, 2025 03:43 UTC
  • Rais wa Zambia atoa wito wa mshikamano na amani Afrika

Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, siku ya Jumapili alitoa wito wa mshikamano wa Kiafrika na maendeleo jumuishi wakati bara la Afrika likiadhimisha miaka 62 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).

Kupitia chapisho kwenye Facebook kwa ajili ya kuadhimisha siku hiyo, Rais Hichilema amesema: “Lazima tunyamazishe bunduki na kuwekeza katika amani. Kutokuwepo kwa utulivu sehemu yoyote ya bara ni tishio kwa kila sehemu. Afrika haiwezi kumudu kugawanyika kwa migogoro ilhali ndoto ya umoja na ustawi ipo karibu."

Hichilema amewaenzi viongozi waanzilishi wa OAU akiwemo Rais wa kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda, Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah. Amesema maono yao ya uhuru, umoja na mshikamano wa Afrika lazima yaendelezwe na kizazi kipya cha viongozi.

Amesema: “Kizazi cha sasa cha viongozi wa Afrika kinapaswa kujitokeza kwa kuweka mbele ukuaji wa uchumi jumuishi, unaoongozwa na uwazi, usimamizi mzuri wa fedha za umma na dhamira ya kuhakikisha maendeleo yanazalisha ajira na fursa kwa Waafrika wote, hususan vijana na wanawake ambao ndio uti wa mgongo wa mustakabali wa bara letu."

Rais Hichilema pia ametoa wito wa mageuzi katika mifumo ya kifedha ya kimataifa ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikizikandamiza nchi za Afrika.

Ameongeza kuwa: “Bara la Afrika lazima liendelee kupigania mfumo wa fedha wa kimataifa ulio na usawa zaidi, mfumo usiokuza tena ukosefu wa usawa wa kihistoria bali unaoiruhusu Afrika kuchagua njia yake ya maendeleo endelevu."

Siku ya  Afrika huadhimisha kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mnamo mwaka 1963, ambao baadaye uligeuka kuwa Umoja wa Afrika wa sasa.