WFP: Watu milioni kumi wakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula DRC
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema kuwa, watu milioni 28 sasa wanakabiliwa na njaa kali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti ya WFP inaeleza kuwa, mashariki mwa DRC, "zaidi ya watu milioni 10 katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tanganyika wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula."
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linatoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Nchi inakabiliwa na mzozo wa chakula ambao haujawahi kushuhudiwa: karibu watu milioni 28 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, idadi ambayo haijawahi kufikiwa na ambayo inaendelea kuongezeka. Katika kipindi cha miezi mitatu pekee, watu wengine milioni 2.5 wamekumbwa na njaa, anaonya mkurugenzi wa kikanda wa WFP Eric Perdison.
Hasa mashariki mwa nchi, katika mikoa iliyoathiriwa na mzozo. Takwimu zinatisha: watu milioni 10 wana uhaba mkubwa wa chakula katika mikoa minne tu ya mashariki mwa DRC - Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri na Tanganyika - na zaidi ya 90% ya kaya katika Kivu Kaskazini na Kusini hawana chakula cha kutosha na wanalazimika kupunguza ukubwa na idadi ya milo yao, na kujinyima chakula chenye lishe bora.
Akizuru Goma wiki iliyopita, Eric Perdison ameelezea kwamba wanakimbizana na wakati ili kumaliza tatizo hili: anahitaji zaidi ya dola za Marekani milioni 400 ili kuendelea na shughuli zake za dharura hadi mwezi wa Oktoba.