Maafisa wa kijeshi wanaoshirikiana na magaidi watiwa mbaroni Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126970-maafisa_wa_kijeshi_wanaoshirikiana_na_magaidi_watiwa_mbaroni_nigeria
Jeshi la Nigeria limewatia mbaroni wanajeshi 18, polisi 15 na raia 8 katika operesheni maalumuu ya kupambana na maafisa wa usalama wanaoshirikiana na magenge ya kigaidi ikiwa ni pamoja na kuwapa silaha magaidi hao.
(last modified 2025-05-29T23:31:58+00:00 )
May 29, 2025 23:31 UTC
  • Maafisa wa kijeshi wanaoshirikiana na magaidi watiwa mbaroni Nigeria

Jeshi la Nigeria limewatia mbaroni wanajeshi 18, polisi 15 na raia 8 katika operesheni maalumuu ya kupambana na maafisa wa usalama wanaoshirikiana na magenge ya kigaidi ikiwa ni pamoja na kuwapa silaha magaidi hao.

Shirika la Habari la Fars limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wakati ukosefu wa usalama unaendelea katika baadhi ya maeneo ya Nigeria kutokana na mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram, jeshi la nchi hiyo limeanzisha msako wa kuwatia mbaroni maafisa wa jeshi, polisi na raia wanaoshirikiana na magaidi hao.

Jeshi la Nigeria limesema katika taarifa yake kwamba, limeendesha operesheni maalumu iliyopewa jina la "Hadin Kai" na kufanikiwa kuwatia mbaroni maafisa kadhaa wa kijeshi na polisi kwa tuhuma za kuyapelekea silaha na risasi magenge ya kigaidi.

Kwa upande wake, tovuti ya "Daily Trust" imeripoti kuwa, watu hao wamekamatwa huku Meja Jenerali Abdulsalam Abubakar, kamanda wa operesheni hiyo akiwashutumu mamluki wa kigeni kwa kuwapa mafunzo wanachama wa Boko Haram na Daesh (ISIS) katika ukanda wa Afrika Magharibi.

Huko nyuma, Babagana Zulum, Mkuu wa Mkoa wa Borno, alikuwa ameonya kuchukuliwa hatua kali magenge ya kijasusi ya kigeni na yeyote atakayebainika kushirikiana na magaidi.

Borno limekuwa moja ya majimbo yasiyo na usalama nchini Nigeria katika miaka ya hivi karibuni na kitovu cha mashambulizi ya Boko Haram. Meja Jenerali Ademola Owelana, afisa mkuu wa jeshi la Nigeria amesema kuwa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wahalifu hao na kwamba operesheni za hivi sasa zimeendeshwa katika majimbo 11.