Milipuko ya kipindupindu yaongezeka Khartoum, Sudan
(last modified Fri, 30 May 2025 07:18:59 GMT )
May 30, 2025 07:18 UTC
  • Milipuko ya kipindupindu yaongezeka Khartoum, Sudan

Serikali ya  Sudan imetangaza ongezeko kubwa la visa vya kipindupindu katika jimbo la Khartoum, ambapo kwa siku moja tu, visa 1,375 vipya vimeripotiwa, na vifo 23 kuthibitishwa.

Akizungumza na vyombo vya habari, Bw. Mohamed Al-Tijani, mkurugenzi wa Dharura na Udhibiti wa Mlipuko katika Wizara ya Afya ya Jimbo la Khartoum, amesema: "Kwa sasa, wagonjwa 1,116 wanapatiwa matibabu katika vituo maalum vya kutenga wagonjwa. Bw. Al-Tijani ameongeza kuwa: "Vituo vya kutenga wagonjwa vimeanzishwa na pia kuna vituo vinne vya makazi ya muda katika maeneo yaliyoathirika zaidi, kwa lengo la kugundua mapema, kutoa tiba kwa haraka, na kupunguza vifo."

Kwa mujibu wa takwimu za awali, siku ya Jumanne kulikuwa na visa 942 vya kipindupindu na vifo 25, huku Jumatatu ikiwa na visa 1,177 na vifo 45.

Kwa ujumla, serikali ya Sudan imeripoti jumla ya visa 60,993 vya kipindupindu kote nchini tangu mlipuko uanze, na vifo 1,632 kuripotiwa hadi sasa.

Ikumbukwe kuwa mwezi Agosti mwaka 2024, mamlaka za Sudan zilitangaza kipindupindu kuwa janga la kitaifa.

Huduma za afya nchini humo zimeporomoka vibaya kutokana na vita vinavyoendelea kati ya jeshi la Sudan na waasi wa kundi la RSF,  vita ambavyo vilianza mwezi Aprili mwaka 2023.

Tokea wakati huo zaidi ya watu 20,000 wameuawa na milioni 15 wamekimbia makazi yao.

Sudan inailaumu serikali ya   Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa inawaunga mkono waasi wa RSF ambao wameitumbukiza nchi hiyo katika vita.