Bamada: Ukraine inaratibu mashambulizi ya magaidi nchini Mali
(last modified Sat, 07 Jun 2025 06:58:48 GMT )
Jun 07, 2025 06:58 UTC
  • Bamada: Ukraine inaratibu mashambulizi ya magaidi nchini Mali

Wakufunzi wa kijeshi wa Ukraine wanawafunza na kuwapa silaha wanamgambo wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda nchini Mali.

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Bamada, makundi ya wanamgambo ambayo yamekuwa yakiendesha uasi dhidi ya serikali katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa zaidi ya muongo mmoja, hivi sasa yanaendeshwa na Ukraine.

Ufichuzi huo ulibainika wazi wakati wa operesheni za hivi majuzi za Wanajeshi wa Mali (FAMa), kufuatia mashambulizi mapya ya kundi la wanamgambo linalojiita Jama’at Nasr al-Islam wal-Muslimin (JNIM), Bamada imeripoti.

Wapiganaji wa JNIM waliripotiwa kushambulia vituo vya usalama huko Sirakorola na Tanabougou, katika mkoa wa kusini-magharibi wa Koulikoro nchini Mali, Mei 30. Kwa mujibu wa kituo hicho, vikosi vya FAMa vilizuia shambulio hilo, na kukamata silaha, nyaraka na vifaa - siku chache baada ya kuwavizia wanamgambo karibu na Djongue Bambara katika eneo la Mto Sofara walipokuwa wakijaribu kutoroka.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop alisema Ukraine inavuruga utulivu barani Afrika kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel barani humo. Katika mahojiano na shirika la habari la RIA Novosti  Diop alisema kuwa, hatua za Ukraine ni tishio kubwa kwa usalama wa kikanda.

Aidha Tatyana Dovgalenko, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alisema karibuni kwamba, silaha za Magharibi zinazotumwa Kiev hatimaye zinaishia mikononi mwa makundi ya kigaidi yenye silaha barani Afrika.