Afisa wa Sudan: Ukraine inafanya ‘kazi chafu’ ya Wamagharibi Afrika
(last modified Mon, 09 Jun 2025 11:13:28 GMT )
Jun 09, 2025 11:13 UTC
  • Afisa wa Sudan: Ukraine inafanya ‘kazi chafu’ ya Wamagharibi Afrika

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan amesema Ukraine inatekeleza "kazi chafu" ya nchi za Magharibi kwa kuunga mkono makundi yenye silaha yanayohusika na mashambulizi ya kigaidi katika mataifa ya Afrika kama vile Libya, Somalia na Niger.

Muhammad Al-Sirr ametoa madai hayo katika mahojiano na Russia Today, ambapo pia ameishutumu Kiev kwa kuwapa silaha waasi wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), ambao wamekuwa kwenye vita vya kikatili na wanajeshi wa Sudan tangu katikati ya Aprili 2023.

"Ushiriki wa Ukraine katika kusaidia makundi mengine nchini Libya, Somalia, na Niger umeanzishwa. Inasaidia makundi kama Boko Haram na al-Shabaab ya nchini Somalia; na nchini Sudan inatoa msaada kwa RSF kwa kuwapa ndege zisizo na rubani, ambazo zinatolewa kwa bei ya kutupa," Al-Sirr amesema. Afisa huyo wa Sudan amedai kuwa, Kiev imekuwa ikisaidia mashambulizi ya RSF dhidi ya miundombinu ya Sudan kwa "karibu miezi saba hadi minane iliyopita."

Haya yanajiri siku chache baada ya kituo cha habari cha Bamada kuripoti kuwa, makundi ya wanamgambo yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na ambayo yamekuwa yakiendesha uasi dhidi ya serikali nchini Mali kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, hivi sasa yanaendeshwa na Ukraine. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop alisema hivi karibuni kuwa, Ukraine inavuruga utulivu barani Afrika kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel barani humo. 

Kadhalika Tatyana Dovgalenko, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alisema karibuni kwamba, silaha za Magharibi zinazotumwa Kiev hatimaye zinaishia mikononi mwa makundi ya kigaidi yenye silaha barani Afrika.