Afrika Kusini yazika miili 30 iliyotelekezwa kwenye mgodi wa dhahabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127432-afrika_kusini_yazika_miili_30_iliyotelekezwa_kwenye_mgodi_wa_dhahabu
Afrika Kusini jana Jumanne ilifanya maziko ya kwanza ya 'kimaskini' ya miili 30 ambayo haikuchukuliwa na jamaa zao, baada ya kupatikana kwenye mgodi wa dhahabu uliotelekezwa huko Stilfontein, mkoa wa Kaskazini Magharibi mwezi Januari mwaka huu.
(last modified 2025-06-11T07:19:04+00:00 )
Jun 11, 2025 07:19 UTC
  • Afrika Kusini yazika miili 30 iliyotelekezwa kwenye mgodi wa dhahabu

Afrika Kusini jana Jumanne ilifanya maziko ya kwanza ya 'kimaskini' ya miili 30 ambayo haikuchukuliwa na jamaa zao, baada ya kupatikana kwenye mgodi wa dhahabu uliotelekezwa huko Stilfontein, mkoa wa Kaskazini Magharibi mwezi Januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Idara ya Afya ya jimbo la Kaskazini Magharibi, Tshegofatso Mothibedi, miili 20 zaidi inatazamiwa kuzikwa mwishoni mwa Juni baada ya kukamilika kwa taratibu zote muhimu za kiutawala.

Amesema, "Pia tumefanikiwa kukabidhi miili 25 kwa wapendwa wao na jamii baada ya kutambuliwa na kuendana na vipimo vya vinasaba DNA."

Mothibedi amenukuliwa akisema hayo na vyombo vya habari vya nchi hiyo na akaongeza kuwa, mazishi ya jana Jumanne yalifanyika katika miji ya Jouberton, Klerksdorp na Kanana jimboni Orkney.

Maiti hizo ni miongoni mwa miili 78 ya wachimbaji migodi 'haramu' walioopolewa mgodini katika operesheni ya serikali. Kufikia Aprili, ni miili 12 pekee iliyokuwa imetambuliwa na wanafamilia. Operesheni hiyo pia iliwapata manusura 246.

Wachimba madini haramu, wanaojulikana kama "zama zamas", wanafanya kazi katika migodi iliyogurwa na sekta ya madini inayodorora ya Afrika Kusini. Watu hao wanafanya kazi bila vibali, mara nyingi katika hali na mazingira hatari, ili kuchimba mabaki ya dhahabu. 

Mwishoni mwa mwaka wa 2023, polisi walianzisha operesheni ya kukomesha kabisa sekta hiyo katika ukanda wa uchimbaji madini wa kaskazini-mashariki mwa Afrika Kusini, na kuzuia vifaa muhimu ili kuwalazimisha watoto kuondoka ndani ya migodi hiyo.