Mahakama Kenya yaiamuru polisi iache kufunga jiji la Nairobi wakati wa maandamano
Mahakama Kuu nchini Kenya imetoa amri ya kuwazuia polisi kuweka vizuizi au kuzuia raia kufika katikati mwa jiji la Nairobi wakati wa maandamano. Jaji wa mahakama hiyo Lawrence Mugambi alitoa amri hiyo jana Jumatano kufuatia kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute baada ya jiji kufungwa wakati wa maandamano ya Saba Saba mnamo Jumatatu wiki hii.
Katika kesi hiyo, Katiba Institute ilisema hatua ya polisi kufunga jiji kwa kutumia nyaya na kuwazuia raia kufika katikati mwa jiji ilikuwa kinyume cha sheria na ukiukaji wa haki na uhuru wao.
“kuna hatari ya Inspekta Jenerali wa Polisi na Mwanasheria Mkuu kuifanya Katiba isiwe na maana yoyote na kubadilisha demokrasia yetu kuwa iliyojaa udikteta,” ilieleza Katiba Institute katika madai yake.
Jaji Mugambi alisema kuwa kesi hiyo ilifaa, akitambua kuwa kuzibwa kwa barabara bila notisi kulivuruga umma mnamo Jumatatu.
“Kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, natoa amri ya kuwazuia Inspekta Jenerali wa Polisi au afisa yeyote dhidi ya kuweka vizuizi na kuwazuia raia kuingia katikati mwa jiji la Nairobi. Hawafai kuweka vizuizi au kuwazuia raia bila kutoa notisi ndipo raia nao wapange shughuli zao mapema,” amesisitiza Jaji Mugambi.
Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, hawakuwa kortini wakati amri hiyo ilikuwa ikitolewa.../