Uchaguzi Tanzania 2025: Watanzania kupiga kura Oktoba 29
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (INEC) Tanzania imetangaza kuwa, uchaguzi mkuu wa mwaka huu (2025), utakaohusisha nafasi ya Rais, wabunge na madiwani, utafanyika siku ya Jumatano, tarehe 29 Oktoba 2025.
Akizungumza katika uzinduzi wa ratiba ya uchaguzi huo jijini Dodoma leo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa rufaa Jacob Mwambegele amesema kuwa, maandalizi ya uchaguzi huo yameanza rasmi na kuainisha tarehe muhimu katika kalenda ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais utafanyika kati ya Agosti 9 hadi 27, 2025. Aidha, ameongeza; "Tarehe 27 Agosti 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha rais na makamu rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani", alisema Jaji huyo.
Kwa upande wa kampeni, Tanzania Bara itakuwa na kipindi cha kampeni kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, huku Tanzania Zanzibar kampeni zikiendeshwa kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 27, ili kupisha upigaji wa kura ya mapema.
"Tarehe 29 Oktoba, 2025 siku ya Jumatano itakuwa ndio siku ya kupiga kura", alisema Mwambegele, kuhusu uchaguzi huo unaolenga kuwapa wananchi fursa ya kidemokrasia kuchagua viongozi wao wa ngazi mbalimbali.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania inatangaza ratiba ya uchaguzi mkuu uujao katika hali ambayo, kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini humo CHADEMA Tundu Lissu anashikiliwa rumande akikabiliwa na kesi ya uhaini.