Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya watu zaidi ya 40 Ituri DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128878-umoja_wa_mataifa_walaani_mauaji_ya_watu_zaidi_ya_40_ituri_drc
Ujumbe wa Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) umelaani vikali shambulio lililotokea Ituri na kupelekea makumi ya watu kuuawa.
(last modified 2025-07-28T23:11:57+00:00 )
Jul 28, 2025 23:11 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya watu zaidi ya 40 Ituri DRC

Ujumbe wa Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) umelaani vikali shambulio lililotokea Ituri na kupelekea makumi ya watu kuuawa.

Takriban raia 43 wamepoteza maisha katika shambulio la usiku lililotokea jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tukio linaloaminika kutekelezwa na waasi wa kikundi cha Allied Democratic Forces (ADF), kinachodaiwa kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la Daesh tawi la kati mwa Afrika.

Washambuliaji walivamia mji wa Komanda, eneo la Irumu, majira ya saa sita usiku wa Jumamosi, wakilenga kundi la waumini waliokuwa wamekusanyika katika ukumbi wa ibada karibu na hospitali kuu ya mji huo. Kwa mujibu wa taarifa, waliouawa walijumuisha waumini wa Kanisa Katoliki waliokuwa wakijiandaa kubatizwa siku ya Jumapili.

Mashahidi walieleza kuwa nyumba zilichomwa moto na mali binafsi kuporwa. Gari la mfanyabiashara kutoka Oicha pia liliunguzwa.

Taarifa hiyo ya MONUSCO iliongeza kusema kuwa , " Kulingana na ripoti rasmi, shambulio la wanajeshi wa ADF lilisababisha vifo vya raia wasiopungua 43 wakiwemo wanawake 19, wanaume 15, na watoto tisa, huku watu kadhaa wakitekwa nyara.

Mashirika ya kiraia ya ndani yametoa wito kwa gavana wa kijeshi kufika Komanda na kuchukua hatua za haraka za kiusalama kuzuia mauaji zaidi. Shambulio hili limefufua mjadala kuhusu hali ya kijeshi, ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka miwili katika eneo hilo lenye mizozo.

Komanda iko katika korido ya kimkakati ya Beni-Bunia, eneo linalojulikana kwa ghasia za mara kwa mara. Mashambulizi kadhaa ya hivi karibuni yameua raia wengi na kuzidisha hali ya ukosefu wa utulivu.