Nchi za Karibiani zawania kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128900-nchi_za_karibiani_zawania_kuimarisha_uhusiano_wa_kibiashara_na_afrika
Nchi za Jumuiya ya Karibiani (CARICOM) zinawania kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika, huku taswira ya biashara ya kimataifa ikibadilika kwa kasi.
(last modified 2025-07-29T07:39:06+00:00 )
Jul 29, 2025 07:39 UTC
  • Nchi za Karibiani zawania kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika

Nchi za Jumuiya ya Karibiani (CARICOM) zinawania kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika, huku taswira ya biashara ya kimataifa ikibadilika kwa kasi.

Katibu Mkuu wa CARICOM, Bi. Carla Barnett, alitoa kauli hiyo Jumatatu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (AfriCaribbean Trade and Investment Forum) uliofanyika Grenada. Amesisitiza kwa kusema: “Ni lazima tufungue mlango kwa uthabiti ili kuwezesha biashara kubwa zaidi kati ya kanda zetu.”

Barnett alieleza haja ya kuvuka kiwango cha sasa ambapo chini ya asilimia 3 ya jumla ya biashara ya CARICOM inafanyika na bara la Afrika.

Wito huu umetolewa wakati ambapo ulinzi wa kibiashara (protectionism) na ushawishi wa kisera kutoka kwa washirika wa jadi, kama vile Marekani, mshirika mkuu wa kibiashara wa CARICOM, vinaongezeka. Hivi karibuni, Washington iliweka ushuru wa asilimia 10 kwa washirika wake wengi wa biashara, sambamba na kushinikiza sera kadhaa katika siasa za ndani za mataifa ya Karibiani.

Ukanda wa Karibiani unachukuliwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyo hatarini zaidi kukumbwa na misukosuko ya kiuchumi duniani, ikiwemo mfumuko wa bei, janga la magonjwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hali hiyo imeongeza umuhimu wa kubadili na kupanua wigo wa uhusiano wa kibiashara.

Barnett pia aligusia ushirikiano unaoendelea kati ya Karibiani na Afrika katika masuala ya kimkakati kama vile kutetea fidia ya kihistoria kwa madhila ya utumwa, pamoja na madai ya fidia kwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Idadi kubwa ya wakaazi wa eneo la Karibiani wana asili ya Afrika, jambo ambalo linatoa msukumo kwao kushirikiana zaidi na nchi za bara Afrika.