Waasi wa M23 wateka vijiji viwili Kongo na kuhatarisha makubaliano ya Doha
Waasi wa M23 wameteka vijiji viwili katika eneo la Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya makubaliano ya amani waliyosainiwa hivi karibuni huko Qatar.
Wapiganaji wa kundi la M23 walividhibiti vijiji viwili vya Ngululu na Ndete katika eneo la Nyamaboko kufuatia mapigano makali siku ya Jumatano kati yao na walinda usalama wa ndani kwa jina la Wazalendo.
Waasi wa M23 walishambulia maeneo ya Wazalendo katika vijiji vyote hivyo viwili. Walinda usalama wa ndani kwa jina la Wazalendo walikimbia baada ya kushtadi mapigano na hivyo kuvitelekeza vijiji hivyo chini ya udhibiti wa waasi wa M23.
Wakazi wa vijiji vya Ngululu na Ndete walikimbia kwa wingi kabla ya kuwasili waasi. Hadi sasa kumeripotiwa mawimbi mawili makuu ya watu waliokimbia makazi yao kufuatia mapigano ya juzi; kundi moja likielekea huko Waloa Yungu katika wilaya ya Walikale na jingine likikimbilia katika kichaka jirani.
Kushtadi mapigano katika jimbo la Kivu kaskazini mashariki mwa Kongo kunauweka hatarini Mkataba wa Doha uliosainiwa hivi karibuni kati ya serikali ya Kongo na waasi wa M23.
Habari zinasema kuwa mapigano yanaendelea katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kati ya waasi wa M23 na wanamgambo walinda usalama kwa jina la Wazalendo, wanaoliunga mkono jeshi la Kongo.