M23, DRC zatia saini makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Qatar
Wawakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 wametia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki mwa DRC, leo Jumamosi nchini Qatar.
Tamko hilo limetiwa saini mjini Doha, mji mkuu wa Qatar, na wawakilishi kutoka pande zote mbili, kufuatia wiki kadhaa za ushirikiano wa kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya awali yaliyofanyika Washington.
Askari wa DRC na waasi wa M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, wamewakabiliano katika mapigano makali, yaliyochochewa na M23 kuteka miji miwili mikubwa zaidi ya DRC, Goma na Bukavu Januari. Mapigano hayo ya Kongo DR yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamia kwa maelfu kuyahama makazi yao.
Kundi la M23, wiki iliyopita lilitaka yafanyike majadiliano zaidi kuzungumzia matatizo ambayo hayakujumuishwa kwenye makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya Rwanda na DRC jijini Washington mwezi Juni.
Makubaliano yaliyofikiwa Washington kati ya DRC na Rwanda yalilenga kumaliza mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DRC.
Tangu mwanzoni mwa Januari 2025, waasi wa M23 wamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na miji ya Goma na Bukavu, na wanaendelea kusonga mbele.
Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wainaishutumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi hao, lakini serikali ya Kigali inakanusha tuhuma hizo na kusema kwamba kundi hilo linafanya kazi chini ya himaya ya serikali ya Kinshasa.