Umoja wa Mataifa: Njaa duniani imepungua lakini bado hali ni mbaya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128954-umoja_wa_mataifa_njaa_duniani_imepungua_lakini_bado_hali_ni_mbaya_afrika
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, kiwango cha njaa duniani kilipungua kidogo mwaka 2024, lakini bado watu zaidi ya milioni 7 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula huku idadi kubwa ikishuhudiwa barani Afrika.
(last modified 2025-07-31T00:44:35+00:00 )
Jul 31, 2025 00:44 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Njaa duniani imepungua lakini bado hali ni mbaya Afrika

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, kiwango cha njaa duniani kilipungua kidogo mwaka 2024, lakini bado watu zaidi ya milioni 7 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula huku idadi kubwa ikishuhudiwa barani Afrika.

Viongozi wa dunia wanapokutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, kwa ajili ya mkutano wa pili wa Mapitio ya Mifumo ya Chakula ya Umoja wa Mataifa (UNFSS+4), wadau wameangazia takwimu za kimataifa zinazoashiria kushuka kwa viwango vya njaa duniani katika miaka ya hivi karibuni, lakini bado watu kati ya milioni 638 na 720 wanakabiliwa na uhaba wa chakula — huku idadi hiyo ikiongezeka zaidi barani Afrika. 

Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kushirikiana na wadau wake wamezindua ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani 2025 (SOFI 2025) inayoangazia mashinikizo yanayoendelea kuathiri upatikanaji wa chakula katika miaka ya hivi karibuni, ambapo mfumuko wa bei ya chakula umetajwa kuwa changamoto kubwa tangu mwaka 2021.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya IFAD, idadi ya watu barani Afrika wasioweza kumudu lishe bora ilipanda na kufikia zaidi ya bilioni 1 mwaka 2024. Inakadiriwa kuwa watu milioni 512 bado watakabiliwa na njaa kufikia mwaka 2030, ambapo karibu asilimia 60 ya hao watakuwa barani Afrika. Rais wa IFAD, Alvaro Lario anasema, “kuongezeka kwa njaa barani Afrika ni jambo la kutia hofu sana na linapaswa kuwa tahadhari kwetu sote, kwani asilimia 20 ya wakazi wa bara hilo wanakabiliwa na utapiamlo, na asilimia 59 hawana uhakika wa chakula.”