Umoja wa Afrika: Hatuitambui serikali sambamba ya Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128956-umoja_wa_afrika_hatuitambui_serikali_sambamba_ya_sudan
Umoja wa Afrika umepinga vikali hatua ya kundi la wanamgambo RSF kutangaza serikali sambamba nchini Sudan, ukisema hatua hiyo inahatarisha umoja wa taifa na juhudi za amani.
(last modified 2025-07-31T00:45:05+00:00 )
Jul 31, 2025 00:45 UTC
  • Umoja wa Afrika: Hatuitambui serikali sambamba ya Sudan

Umoja wa Afrika umepinga vikali hatua ya kundi la wanamgambo RSF kutangaza serikali sambamba nchini Sudan, ukisema hatua hiyo inahatarisha umoja wa taifa na juhudi za amani.

Umoja wa Afrika kupitia Baraza lake la Amani na Usalama umetangaza kutoutambua utawala uliotangazwa na kundi la Rapid Support Forces, RSF, na washirika wake, katika maeneo wanayoyadhibiti magharibi na kusini mwa Sudan.

Umoja huo umezitaka nchi wanachama na jumuiya ya kimataifa kutounga mkono kile kilichoitwa ''serikali nyingine iliyotangazwa na RSF,'' ikisema inauweka rehani mustakabali wa taifa hilo.

Tangazo la RSF la kuunda serikali sambamba lilitolewa tarehe 27 Julai, na kupokelewa kwa upinzani si tu kutoka kwa Umoja wa Afrika, bali pia Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, na Saudi Arabia. Wote wametoa msimamo wa kuitambua tu serikali ya kiraia iliyoanzishwa mjini Port Sudan, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Kamil Idris.

Wakati huo huo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imelaani vikali tangazo la kuundwa serikali sambamba na Vikosi vya Msaada wa Haraka vinavyoongozwa na "Mohammed Hamdan Dagalo", anayejulikana kwa jina la "Hemedti".

Zaidi ya watu 25,000 wameuawa na zaidi ya milioni 10 wamekimbia makazi yao tangu Aprili 2023, wakati vita vya kuwania madaraka vilipozuka kati ya Jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na wanamgambo wa kikosi cha RSF wanaoongozwa na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo.