Marais Ruto, Museveni waikosoa Tanzania kwa kuongeza vikwazo vya biashara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128966-marais_ruto_museveni_waikosoa_tanzania_kwa_kuongeza_vikwazo_vya_biashara
Rais William Ruto wa Kenya na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni wametangaza kwa pamoja kwamba vizingiti vya kibiashara kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) vinaathiri maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
(last modified 2025-07-31T03:30:55+00:00 )
Jul 31, 2025 03:30 UTC
  • Marais Museveni na William Ruto
    Marais Museveni na William Ruto

Rais William Ruto wa Kenya na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni wametangaza kwa pamoja kwamba vizingiti vya kibiashara kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) vinaathiri maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa pamoja katika Ikulu ya Nairobi jana Jumatano, viongozi hao wawili walieleza wasiwasi wao kuhusu baadhi ya mataifa kukataa kufungua masoko yao kwa nchi wanachama katika umuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hali ambayo imesababisha mlolongo wa vizuizi vinavyokwamisha biashara huru.

Viongozi hao walikutana kujadili masuala ya biashara, usalama na amani ya kikanda. Mkutano wao umefanyika wakati ambapo vizingiti visivyo vya ushuru vimeongezeka licha ya uwepo wa fursa kubwa ya biashara katika ukanda huo.

Rais Museveni alisema ukanda wa Afrika Mashariki unapaswa “kuamka” na kufanya maamuzi ya busara kuhusu biashara na uchumi. Alitarajiwa kutoa mhadhara wa hadhara katika Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi (NDC), mjini Nairobi.

Kwa upande wake, Rais William Ruto amesema walijadili “vizingiti sugu visivyo vya ushuru vinavyokwamisha uhamishaji wa bidhaa na kudhoofisha malengo ya ujumuishaji wa kikanda chini ya mfumo wa EAC.”

Ingawa hawakutaja nchi mahsusi, lakini mkutano huo umefanyika baada ya Tanzania kuchafua mkataba wa soko la pamoja kwa kupiga marufuku wageni kushiriki katika shughuli 15 za kiuchumi zinazochukuliwa kama biashara ndogo. Tanzania ilisema ilikuwa ikiwalinda wananchi wake dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka kwa wageni – japo raia wake wana fursa sawa katika mataifa mengine ya EAC.

Tanzania pia ilirudisha ushuru wa viwanda kwa bidhaa zinazozalishwa katika nchi wanachama, jambo linaloonekana kuvunja kanuni ya ushuru wa pamoja wa nje unaolenga kulinda ukanda huu na kuchochea ukuaji wa viwanda vyake.