Angola: 22 wameuawa katika ghasia za kupinga ongezeko la bei ya mafuta
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Angola ametangaza kuwa watu 22 wameaga dunia na zaidi ya 1,000 wamekamatwa kutokana na ghasia zilizosababishwa na maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta. Watu wengine wasiopungua 197 wamejeruhiwa katika machafuko hayo.
Machafuko hayo yalizuka siku ya Jumatatu wakati vyama vya mabasi madogo vilipoanzisha mgomo wa siku tatu dhidi ya uamuzi wa serikali wa kuongeza bei ya dizeli kwa thuluthi moja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia ruzuku za gharama kubwa na kuimarisha fedha za bajeti ya umma.
Uporaji, uharibifu na mapigano ya waandamanaji na polisi yalianza katika mji mkuu, Luanda, na kisha kuenea katika majimbo mengine sita ya Angola.
Milio ya risasi ya hapa na pale ilisikika Luanda na miji mingine kadhaa siku za Jumatatu na Jumanne huku watu wakipora maduka na kukabiliana na polisi.
Baraza la mawaziri la Rais Joao Lourenco wa Angola lilikutana jana Jumatano na kupokea ripoti kuhusu hali ya usalama na hatua zilizochukuliwa na polisi kukabiliiana na machafuko hayo.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais imesema kumeripotiwa vifo vya watu 22, watu 197 wamejeruhiwa na 1,214 wamekamatwa. Maduka 66 na magari 25 yameharibiwa, na baadhi ya maduka makubwa na maghala yameporwa, ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa jeshi limetumwa kurejesha utulivu kwa sababu ghasia hizo "zimesababisha hali ya ukosefu wa usalama".
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Angola, Manuel Homem amewaambia waandishi wa habari kuwa afisa wa polisi alikuwa miongoni mwa watu 22 waliouawa.
Mitaa ya Luanda ilitawaliwa na hali ya wasiwasi na ilikuwa tupu kwa kiasi kikubwa jana Jumatano, ingawa kulikuwa na foleni nje ya vituo vya mafuta na baadhi ya maduka.
Angola ambayo ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika baada ya Nigeria, inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Taarifa ya Mamlaka ya Taifa ya Takwimu inaonyesha kuwa mfumuko wa bei unaongezeka kwa 20% na ukosefu wa ajira kwa 30%.