WFP: Kupunguzwa misaada Nigeria kuwatumbukiza vijana mikononi mwa Boko Haram
Imeelezwa kuwa, kupunguzwa misaada ya kibinadamu kaskazini-mashariki mwa Nigeria kunaweza kuwa faida kwa moja ya makundi hatari zaidi ya kigaidi ulimwenguni, Boko Haram.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeeleza kuwa, itakuwa rahisi zaidi kwa wanamgambo kuwarubuni vijana kujiunga nao na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo lote.
Likiwa kundi maarufu duniani kote kwa kuwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule kutoka mji wa Chibok zaidi ya muongo mmoja uliopita, Boko Haram liliwateka maelfu ya watu wakati wa uvamizi wao na kuwalazimisha zaidi ya milioni moja kutoka kwa makazi yao ya vijijini.
Kundi la kigaidi la Boko Haram, ambalo limekuwa likiendesha hujuma za kigaidi nchini Nigeria tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, limehusika na mashambulizi ya kigaidi ya kutisha tangu mwaka 2009, na kupelekea maelfu kupoteza maisha.
Nigeria imekuwa ikikabiliana na hujuma za makundi ya kigaidi yenye silaha kwa muda wa miaka 16 huko kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo; hujuma ambazo kimsingi zinatekelezwa na Boko Haram na tawi lake la ISWAP na zimesababisha hasara kubwa kwa binadamu na uchumi, ikiwa ni pamoja na watu wengi kulazimika kuhakama makazi yao na mgogoro wa binadamu.
Ghasia za Boko Haram, zilizoanzia kaskazini-mashariki mwa Nigeria, zimevuka mipaka na kuathiri mataifa jirani ya Cameroon, Chad na Niger—zikisababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni kukimbia makazi yao.