Bobi Wine: Mazingira ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu Uganda hayafai
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssntenamu, almaarufu kama Bobi Wine amesema kuwa, mazingira ya kisiasa nchini humo yamekuwa mabaya zaidi kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mapema mwaka ujao (2026).
Bobi Wine amesema amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa kwenye makao makuu ya chama chake cha National Unity Platform, mjini Kampala na kubainisha kwamba, kumekuwa na vitisho dhidi ya maisha yake na wanaharakati wengine wanaohamasisha upinzani dhidi ya rais aliyekaa muda mrefu nchini humo Yoweri Museveni.
"Hali imezidi kuwa mbaya zaidi kwa kila upande ambapo vitisho dhidi ya maisha yangu vimeongezeka, pamoja na utekaji nyara, kukamatwa kwa watu, na hata mauaji. Kwa mfano, kaka mmoja huko Karamoja alipigwa risasi zaidi ya 150. Lengo ni kuwatisha wale wanaoshirikiana nami na wanaoamini katika misimamo yangu. Lakini badala yake, upinzani wetu umeimarika: Wanachama wameongezeka, watu wanazungumza zaidi, na dhamira yetu imekuwa thabiti zaidi."
Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulani Ssentamu amesema kama mpinzani mkubwa wa Museveni, amekuwa na wasiwasi unaozidi kuongezeka katika kipindi cha karibuni, unaochochewa zaidi na mashambulizi kutoka kwa mtoto wa Museveni na Mkuu wa Majeshi Muhoozi Kainerugaba kupitia mtandao wa X.
Mwezi Januari, Kainerugaba aliandika kwamba atamkata kichwa Wine ikiwa rais atamruhusu kufanya hivyo. Na kama haitoshi, mwezi Mei alitoa matamshi yaliyoibua ukosoaji mkubwa aliposema alikuwa akimshikilia mlinzi wa Wine, ambaye alikuwa amepotea. Mlinzi huyo siku chache baadae alionekana akiwa mahakamani lakini akiwa hawezi kutembea bila ya kusaidiwa.