Maandamano Angola: Umoja wa Mataifa watoa wito wa uchunguzi kuhusu vifo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129038-maandamano_angola_umoja_wa_mataifa_watoa_wito_wa_uchunguzi_kuhusu_vifo
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande husika nchini Angola kujizuia na kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vya usalama.
(last modified 2025-08-01T23:10:39+00:00 )
Aug 01, 2025 23:10 UTC
  • Maandamano Angola: Umoja wa Mataifa watoa wito wa uchunguzi kuhusu vifo

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande husika nchini Angola kujizuia na kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vya usalama.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeitaka mamlaka ya Angola kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina na ulio huru kuhusu vifo hivyo na kile kilichoripotiwa kama matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano hayo.

"Picha ambazo hazijathibitishwa zinaonyesha kuwa vikosi vya usalama vilitumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji, zikionyesha matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima na yasiyo na uwiano," amesema Thameen Al-Kheetan, msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa.

Watu 22 wanaripotiwa kuaga dunia na zaidi ya 1,000 wamekamatwa kutokana na ghasia zilizosababishwa na maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta. Watu wengine wasiopungua 197 wamejeruhiwa katika machafuko hayo. Machafuko hayo yalizuka siku ya Jumatatu wakati vyama vya mabasi madogo vilipoanzisha mgomo wa siku tatu dhidi ya uamuzi wa serikali wa kuongeza bei ya dizeli kwa thuluthi moja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia ruzuku za gharama kubwa na kuimarisha fedha za bajeti ya umma.

Uporaji, uharibifu na mapigano ya waandamanaji na polisi yalianza katika mji mkuu, Luanda, na kisha kuenea katika majimbo mengine sita ya Angola. Baraza la mawaziri la Rais Joao Lourenco wa Angola lilikutana siku ya Jumatano na kupokea ripoti kuhusu hali ya usalama na hatua zilizochukuliwa na polisi kukabiliiana na machafuko hayo.