Jamii ya Wangazija yapiganiwa itambuliwe rasmi nchini Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129302-jamii_ya_wangazija_yapiganiwa_itambuliwe_rasmi_nchini_kenya
Seneta wa Kaunti ya Mombasa iliyoko eneo la pwani ya Kenya ametoa wito wa kutaka suala la jamii ya Wangazija kutatuliwa na kupewa haki kama watu wengine nchini humo.
(last modified 2025-08-08T11:39:37+00:00 )
Aug 08, 2025 11:39 UTC
  • Jamii ya Wangazija yapiganiwa itambuliwe rasmi nchini Kenya

Seneta wa Kaunti ya Mombasa iliyoko eneo la pwani ya Kenya ametoa wito wa kutaka suala la jamii ya Wangazija kutatuliwa na kupewa haki kama watu wengine nchini humo.

Mohammed Faki amesema: “hawa Wangazija wanazungumza Kiswahili na wanaishi katika maeneo ya pwani ya Kenya, hasa katika kaunti ya Mombasa. Licha ya mchango wao wa kiutamaduni na kidini katika eneo hilo, bado wanaendelea kutengwa”.

Kwa mujibu wa Faki, kutoitambua jamii hiyo rasmi kunawanyima fursa watu wake ya kupata huduma muhimu za serikali, na uwakilishi katika taasisi za umma pamoja na kujumuishwa katika mipango mikakati ya kuimarisha maisha ya jamii ndogo ndogo.

Seneta huyo wa Kaunti ya Mombasa amebainisha kuwa hilo ni kinyume na Katiba ya Kenya ambayo inahimiza usawa na kujumuisha watu.

Aidha, ametaka kufahamu kama kuna hatua zozote zinazoangaziwa na taasisi za serikali katika kuwatambua rasmi watu wa jamii ya Wangazija.

Faki ametaka pia jamii hiyo ijumuishwe katika sensa za taifa, uteuzi wa nafasi za umma na miradi ya maendeleo inayolenga jamii zilizotengwa.

Jamii ya Wangazija ambayo imekuwepo katika maeneo ya Mombasa kwa muda mrefu, haijatambuliwa kama moja ya makabila nchini Kenya, licha ya mchango wake kihistoria.

Asili ya Wangazija wanatoka visiwa vya Comoro.../