Kenya yapuuzilia mbali vitisho vya US kwa sababu ya uhusiano wake wa kibiashara na Iran na Russia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129328
Serikali ya Kenya, kupitia Mkuu wa Mawaziri, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Musalia Mudavadi imepuuza tishio kwamba Marekani huenda ikaifutia hadhi maalumu ya uhusiano na kusisitiza kuwa, ina haki ya kufanya biashara na nchi tofauti duniani.
(last modified 2025-08-09T06:58:10+00:00 )
Aug 09, 2025 06:58 UTC
  • Kenya yapuuzilia mbali vitisho vya US kwa sababu ya uhusiano wake wa kibiashara na Iran na Russia

Serikali ya Kenya, kupitia Mkuu wa Mawaziri, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Musalia Mudavadi imepuuza tishio kwamba Marekani huenda ikaifutia hadhi maalumu ya uhusiano na kusisitiza kuwa, ina haki ya kufanya biashara na nchi tofauti duniani.

Hio ni kufuatia ripoti kuwa Seneta mmoja wa Marekani amependekeza Washington ichunguze na kutathmini uhusiano wake na Kenya.

Mudavadi amethibitisha hayo wakati kuna muswada unaopendekezwa katika Seneti ya Marekani ukitishia kufuta hadhi ya nchi hiyo isiyo ya NATO (MNNA) kutokana na uhusiano wake wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia.

Akizungumza mbele ya kamati ya Bunge siku ya Alkhamisi, mkuu huyo wa mawaziri na waziri huyo wa mambo ya nje alipuuza madai kwamba uhusiano wa kidiplomasia wa Kenya na Tehran na Moscow ni wa hatari kwa Nairobi.

“Tuna uhusiano na Iran kwa sababu ni wanunuzi wakubwa wa chai yetu. Kama serikali tuna jukumu la kutafuta soko kwa wakulima wetu wa chai, lazima tuuze kahawa, na maua yetu. Kwa hiyo ni lazima kutafuta soko,” alisisitiza Mudavadi .

Amebainisha kuwa, inachofanya serikali ni kutumia tu haki yake kuu ya kutafuta fursa za kiuchumi kwa wakulima na wafanyabiashara wake.

Mudavadi aliiambia kamati hiyo:"kuna upotoshaji kuhusu baadhi ya masuala haya. Kenya ni nchi huru na lazima iwe huru kushirikiana na taifa lolote kwa maslahi ya watu wake",

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mfumo wa Marekani wa biashara na nchi nyengine unaoitwa AGOA unafikia kikomo mwaka huu 2025, na haijulikani kama Washington, chini ya serikali ya sasa ya Trump itaendelea nao mpango huo.../