WHO: Ugonjwa wa malale si tatizo tena la afya ya umma Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129378
Kenya imefanikiwa kutokomeza rasmi ugonjwa wa malale ambao ulionekana kama tatizo la afya ya umma.
(last modified 2025-08-10T10:42:32+00:00 )
Aug 10, 2025 10:41 UTC
  • WHO: Ugonjwa wa malale si tatizo tena la afya ya umma Kenya

Kenya imefanikiwa kutokomeza rasmi ugonjwa wa malale ambao ulionekana kama tatizo la afya ya umma.

Hayo yameelezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) Kwa muktadha huo, Kenya inakuwa nchi ya kumi duniani kufikia mafanikio hayo muhimu ya kiafya.

Kwa mujibu wa WHO, ugonjwa huo ambao unaitwa rasmi trypanosomiasis ya Kiafrika ya binadamu (HAT), umeenea katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara na kwa kawaida unaua ikiwa hakutapatikana matibabu ya kutosha.

Taarifa ya WHO Kanda ya Afrika iliyotolewa katika miji ya Brazaville, Congo na Nairobi, Kenya inasema malale ni ugonjwa wa tropiki unaosababishwa na vimelea vya damu vya Trypanosoma brucei, na huenezwa kwa binadamu kwa kung’atwa na mbung’o waliombukizwa vijidudu hivyo.

Aina ya ugonjwa wa malale uliokuwepo Kenya ni Rhodesiense, ambao huenea haraka na huathiri vibaya viungo mbalimbali, ukiwemo ubongo, na bila matibabu, huweza kusababisha kifo ndani ya wiki chache.

"Ninaipongeza serikali na raia wa Kenya kwa mafanikio haya ya kihistoria," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, alinukuliwa katika taarifa. "Kenya inaungana na idadi inayoongezeka ya nchi ambazo zimetokomeza HAT. Hii ni hatua nyingine ya kutokomeza magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika barani Afrika."

Mbali na Kenya, nchi zingine ambazo zimeondoa ugonjwa wa usingizi kama tatizo la afya ya umma ni Benin, Côte d'Ivoire, Ghana, Guinea, Equatorial Guinea, Uganda, Rwanda, Chad na Togo.

Hii ni habari njema kwa mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa vimelea, lakini hatupaswi kuridhika, anasema Dk Augustin Kadima Ebeja. Meneja huyu wa magonjwa ya malale katika Ofisi ya WHO kanda ya Afrika, yenye makao yake makuu mjini Brazzaville, anaonya kwamba "tulishuhudia hali kama hiyo katika miaka ya 1960, ambapo ugonjwa huo ulikuwa karibu sifuri, lakini ukaongezeka tena."