HRW: Waasi wa M23 wameuwa raia zaidi ya 140 mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129768-hrw_waasi_wa_m23_wameuwa_raia_zaidi_ya_140_mashariki_mwa_kongo
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeeleza hii leo kuwa waasi wa kundi la M23 limeuwa raia zaidi ya 140 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-08-20T11:58:21+00:00 )
Aug 20, 2025 11:58 UTC
  • HRW: Waasi wa M23 wameuwa raia zaidi ya 140 mashariki mwa Kongo

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeeleza hii leo kuwa waasi wa kundi la M23 limeuwa raia zaidi ya 140 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mauaji hayo yalitekelezwa katika vijiji visivyopungua 14 na katika maeneo ya mashamba karibu na Hifadhi ya Taifa ya Virunga kati ya Julai 10 na 30 mwaka huu. 

"Ripoti za kuaminika zinaonyesha kuwa idadi ya watu waliouawa katika eneo la Rutshuru tangu Julai 10 mwaka huu inaweza kupindukia 300. Mauaji haya yanatajwa kuwa kati ya ukatili mbaya zaidi kuwahi kufanywa na waasi wa M23 tangu kuibuka tena kwa uasi wa kundi hilo mwishoni mwa mwaka 2021.

Taarifa ya Shirika la Human Rights Watch imeongeza kuwa wahanga wa mauaji hayo ni pamoja na wakazi na wakulima wakiwemo watoto na wanawake ambapo waliuawa katika vijiji vyao, mashambani na karibu na Mto Rutshuru. 

Ukinukuu watu walioshuhudia, Umoja wa Mataifa na vyanzo vya kijeshi vimeripoti kuwa, jeshi la Rwanda pia "lilihusika katika operesheni za waasi wa kundi la M23."

Clementine de Montjoye Mtafiti wa ngazi ya juu wa Eneo la Maziwa Makuu katika shirika la Human Rights Watch amesema kuwa kundi la waasi la M23 ambalo linadaiwa kuungwa mkono na Rwanda lilishambulia vijiji zaidi ya 12 na mashamba kadhaa mwezi Julai mwaka huu na kufanya mauaji ya kiholela dhidi ya raia wa Kihutu. 

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu liliwahoji pia watu 36 wakiwemo mashuhuda 25 pamoja na wanaharakati wa ndani, wafanyakazi wa sekta ya afya, wanajeshi na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na kuchambua  video na picha mbalimbali kuhusu mauaji hayo.

HRW imetoa ripoti hii mkabala wa kuhahirishwa makubaliano ya amani kati ya serikali ya Kongo na waasi wa M23.