Serikali ya Eswatini inakabiliwa na kesi mahakamani kuhusu watu waliofukuzwa Marekani
Kundi la mawakili watetezi wa haki za binadamu na taasisi zisizo na kiserikali (NGOs) linaishtaki serikali ya Eswatini kwa kukubali kuwapa hifadhi watu watano waliofukuzwa nchini Marekani.
Mawakili hao wamesema kuwa, mapatano ya nyuma ya pazia (siri) kati ya serikali ya Eswatini na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kuwapokea wahamiaji wa nchi ya tatu ni kinyume na Katiba.
Katika pingamizi lao la kisheria, kundi la mawakili watetezi wa haki za binadamu wa Eswatini wamesema kuwa serikali ya nchi hiyo imekiuka taratibu za kisheria kwa sababu mpango huo wa kuwapokea raia waliofukuzwa Marekani haukuwasilishwa bungeni ili kuidhinishwa na wabunge.
Wameongeza kuwa, jela ambayo raia hao watano kutoka Marekani wanashikiliwa imezidiwa uwezo kwa asilimia 190 na kwamba wameshindwa kuonana na raia hao kutoka Marekani. Raia hao kutoka Vietnam, Jamaica, Laos, Yemen na Cuba ambao Washington imesema ni wahalifu hatari, walisafrishwa hadi nchini Eswatini huko kusini mwa Afrika mwezi Julai mwaka huu.
Serikali ya Eswatini kwa upande wake imesema imewaweka katika kifungo cha upweke hadi watakapofanikiwa kuwawerejesha makwao.
Wananchi wa Eswatini wamekasirishwa na kushikiliwa raia hao waliofukuzwa Marekani katika kituo cha Matsapha. Nchi hiyo inaongozwa na Mfalme Mswati III.
Mfalme Mswati awali alitamka kuwa watu hao waliofukuzwa Marekani si tisho na kwamba makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Eswatini na Marekani ni matokeo ya uhusiano mwema kati ya nchi hiyo na Washington.