Kampuni ya Mafuta ya Serikali ya Nigeria: Wizi wa mafuta kupitia mabomba wakaribia kukomeshwa
Kampuni ya mafuta ya serikali ya Nigeria (NNPC Limited) imeripoti kuwa karibu wizi wote wa mafuta uliokuwa ukifanywa kupitia mabomba umekaribia kukomeshwa, baada ya juhudi zilizoratibiwa na mashirika ya ulinzi na intelijensia ya nchi hiyo.
Miaka mitatu iliyopita, ni kiasi cha asilimia 30 tu ya mafuta yaliyokuwa yamesafrishwa kupitia mabomba ya mafuta ndio yaliyofika katika vituo vya vya Nigeria vya uuzaji nje mafuta; na hivyo kupelekea kupotea mabilioni ya fedha mapato ya serikali na kusababisha kuakhirisha shughuli za uwekezaji.
Akizungumza katika Kongamano la Kikanda la Usalama huko Abuja, Bayo Ojulari Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Nigeria amesema kuwa leo hii anaweza kueleza kwa fakhari kuongezeka kwa mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta nje ya nchi.
Amesema, usalama umeimarishwa hivi sasa hasa ndani ya jimbo la Niger Delta, ambapo kuna miundombinu mingi ya mafuta ya nchi.
Uzalishaji wa mafuta nchini Nigeria mara ya mwisho mwaka 2005 ulikaribia mapipa milioni 2.5 kwa siku kabla ya wanamgambo katika jimbo la Delta kupelekea kupungua uzalishaji na kufikia mapipa milioni 1 mwaka 2016.
Mwaka 2021 Nigeria ilianza kuajiri makampuni ya usalama ya binafsi ili kusaidia mashirika ya usalama wa taifa kusimamia usalama wa mabomba ya kusafirisha mafuta.
Afisa Mkuu wa Mtendaji wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Nigeria amesema: Biashara haramu ya mafuta haikuwa tu tatizo la ndani lakini biashara hiyo iliyahusisha pia "makampuni mbalimbali ya kimataifa yaliyotumia udhaifu katika mifumo ya usalama ya kitaifa na kikanda.