Waasi wenye silaha wauwa watu wasiopungua 32 kaskazini mwa Nigeria
-
Polisi ya Nigeria katika mapambano dhidi ya wahalifu wenye silaha
Watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki wamevamia vijiji vitatu kaskazini mwa Nigeria, na kuua takriban watu 32 na kuwateka nyara wengine kadhaa.
Mashambulizi hayo yaliripotiwa jana katika eneo la Borgu katika jimbo la Niger huku kukiwa na tatizo kubwa la usalama kaskazini mwa Nigeria, likiyahusisha na makundi ya wanamgambo wenye silaha yenye mfungamano na kundi la ISIS au Daesh, na pia magenge mengine ya uhalifu yanayowateka nyara watu ili kupewa kikomboleo.
Wasiu Abiodun, Msemaji wa Polisi wa Jimbo la Niger, kaskazini mwa Nigeria, amethibitisha kujiri shambulio katika kijiji kimoja. Amesema, watu wanaoshukiwa kuwa majambazi walishambulia kijiji cha Tunga-Makeri na kuuwa watu sita.
Majambazi hao aidha walichoma moto nyumba kadhaa na hadi sasa haijajulikana ni raia wangapi waliotekwa nyara katika shambulio hilo.
Baada ya kufanya uhalifu katika kijiji cha Tunga-Makeri; watu hao waliokuwa na silaha walielekea katika kijiji cha Konkoso. Jeremiah Timothy mkazi wa kijiji cha Konkoso ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanamgambo waliokuwa na silaha walikivamia kijiji chao mapema jana na kufyatua ovyo risasi.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Konkoso amesema: Watu wasiopungua 26 wameuawa hadi sasa katika kijiji hicho baada ya watu waliokuwa silaha kukichoma moto kituo cha polisi.