Vita vya Sudan: Wapiganaji 318 wa RSF wajiunga na jeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140810-vita_vya_sudan_wapiganaji_318_wa_rsf_wajiunga_na_jeshi
Jeshi la Sudan limeripoti kuwa wapiganaji 318 wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), wakiwemo makamanda wanne wameasi na kujiunga na jeshi hilo katika tukio la hivi karibuni la wanachama wa kikosi hicho cha kijeshi kuamua kujisalimisha.
(last modified 2026-08-20T03:28:22+00:00 )
Aug 20, 2026 03:21 UTC
  • Wapiganaji 318 wa RSF wajiunga na jeshi la Sudan
    Wapiganaji 318 wa RSF wajiunga na jeshi la Sudan

Jeshi la Sudan limeripoti kuwa wapiganaji 318 wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), wakiwemo makamanda wanne wameasi na kujiunga na jeshi hilo katika tukio la hivi karibuni la wanachama wa kikosi hicho cha kijeshi kuamua kujisalimisha.

Hatua hii inakuja huku visa vya uasi vikiongezeka na mapigano yakiendelea kuigubika Sudan kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Maafisa wa Sudan wamesema kuwa wanamgambo 318 wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) cha Sudan, wakiwemo makamanda wanne wa kundi hilo wamejiunga na jeshi la Sudan.

Taarifa zinasema kuwa kundi hilo liliwasili likiwa na hadi magari 50 ya kivita na kutangaza uamuzi wake wa kujiunga na jeshi la Sudan katika eneo la Al-Dabba, katika Jimbo la Kaskazini.

Kamanda wa Walinzi wa Mpaka, Mohamed Saleh Younes amesema kuwa jeshi litawakaribisha wale watakaochagua kurejea katika safu zake, kwamba vikosi vya jeshi vitaendeleza juhudi za kurejesha usalama

Luteni Kanali Musa Ali Ahmed, aliyetambuliwa kama kiongozi wa walioasi, ameuhusisha uamuzi wao huu na kile alichokitaja kuwa ni ukosefu wa mifumo ya kitaasisi ndani ya RSF.

Amesema wamechagua kujiunga na jeshi la Sudan lengo likiwa ni kudumisha umoja nchini humo.

Jeshi la Sudan na wanamgambo wa kikosi cha RSF wamekuwa katika  mzozo mkali wa kuania madaraka tangu mwezi Aprili mwaka 2023, ambapo hadi  pande hizo zimeshindwa kufikia suluhu ya kudumu ya kisiasa.