Rais wa Rwanda akadhibisha ripoti zinazolihusisha jeshi na mauaji mashariki mwa Kongo
-
Rais Paul Kagame
Rais Paul Kagame wa Rwanda amekadhibisha ripoti kwamba jeshi la nchi hiyo lilihusika katika mauaji mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kagame ambaye alikuwa akizungumza mbele ya hadhara ya jeshi na vikosi vya polisi katika kambi ya mafunzo mashariki mwa Rwanda amesema kuwa: Vitendo vya ukatili mashariki mwa Kongo vinafanywa na wanamgambo wa kikosi cha FDLR wenye mfungamano na serikali ya Kongo, wapiganaji kwa jina la Wazalendo na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Matamshi haya ya Rais Kagame yanafuatia ripoti za mapema mwezi huu za Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na Shirika la Haki za Kibinadamu zilizolihusisha Vikosi vya Ulinzi vya Rwanda (RDF) na mauaji ya raia mashariki mwa Kongo.
Mwezi Januari mwaka huu, zaidi ya mamluki 200 wa Ulaya, ambao walidaiwa kupigana upande wa jeshi la Kongo katika vita dhidi ya waasi wa M23, walisafirishwa hadi katika nchi zao za asili kupitia nchi jirani ya Rwanda.
Wapiganaji hao walijisalimisha katika kambi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) nchini Kongo kwa ajili ya usalama wao baada ya waasi wa M23 kuuteka mji wa kimkakati wa Goma.