Rais wa Sudan Kusini atuhumiwa kwa upendeleo baada ya kumteuwa binti yake katika cheo cha juu serikalini
-
Salva Kiir
Adut Salva Kiir, binti wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ameteuliwa na baba yake kuwa Mjumbe wa Rais Anayehusika na Mipango Maalumu, kazi ambayo awali ilikuwa inafanywa na Makamu wa Rais wa sasa.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi kubwa za Rais wa Sudan Kusini za kuimarisha nguvu zake na kuanziisha utawala wa kisiasa wa kiukoo.
Adut Salva Kiir hajawahi kushika wadhifa wowote serikalini, na amekuwa akijishughulisha na masuala ya kibinadamu kupitia taasisi yake ya Adut Salva Kiir Foundation.

Katika ujumbe wake mpya aliotuma katika mtandao wa kijamii, binti huyo wa Rais wa Sudan Kusini amesema kuwa atahudumu kama mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Rais.
Akizungumza katika mahojiano na Redio Tamazuj leo Jumatano, James Boboya mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Sudan Kusini amesema kuwa hatua ya Rais Salva Kiir ya kumteuwa binti yake ni kuelekea katika kile alichokiita kuwa ni "utawala wa urithi,” ambapo viongozi hujaribu kuweka mamlaka kati na kugawanya rasilimali ndani ya duara dogo la ndani.
Makundi ya kiraia ya Sudan Kusini pia yamemhimiza Adut Kiir kutoa kipaumbele kwa maslahi ya umma.