UNICEF yaonya: Watoto wamenasa kwenye janga la kutisha El Fasher, Sudan
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limeonya juu ya janga kubwa la kuogofya linalowawajihi watoto walionasa mjini El-Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan.
UNICEF imesema, takriban raia 260,000, wakiwemo watoto 130,000, wamesalia katika hali mbaya baada ya zaidi ya miezi 16 ya kukatwa misaada mjini El Fasher. Idadi hiyo ya watoto imeelezwa na UNICEF kuwa janga kubwa la kutisha, huku kesi zaidi ya 1,100 za ukiukaji mkubwa wa haki za watoto hao zikithibitishwa tangu mji huo uwe chini ya mzingiro mnamo Aprili 2024.
Kwa mujibu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watoto 1,000 wameuawa au kusababishiwa ulemavu wa daima wakiwa majumbani mwao, kambini, au masokoni. Takriban watoto 23 wamekumbana na ukatili wa kingono, huku wengine wakitekwa nyara au kuandikishwa na makundi yenye silaha.
Hivi karibuni, watoto saba waliripotiwa kuuawa katika shambulio dhidi ya kambi ya wahamiaji ya Abu Shouk mjini El Faher. Mji wa El-Fasher umekuwa kitovu cha mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na waasi wa RSF tangu Mei 2024, licha ya tahadhari za kimataifa kuhusu hatari za ghasia katika mji huo ambao ni kitovu muhimu cha kibinadamu kwa majimbo matano ya Darfur.
UNICEF inahimiza upatikanaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu na ulinzi kwa raia wa mji huo wakiwemo watoto wadogo. Nao Mtandao wa Madaktari wa Sudan umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuwashinikiza vinara wa RSF wasitishe mauaji ya kimbari, njaa ya makusudi, mashambulizi ya makombora na mzingiro dhidi wa mji El-Fasher.
Mji wa El-Fasher umekuwa chini ya mzingiro tangu Mei, na mashirika ya ndani ya Sudan yanawalaumu waasi wa RSF kwa kushambulia maeneo ya raia licha ya wito wa kimataifa wa kulinda miji.