Wanamgambo wa RSF washambulia hospitali jimboni Darfur; watu 12 wameuawa, 17 kujeruhiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131782-wanamgambo_wa_rsf_washambulia_hospitali_jimboni_darfur_watu_12_wameuawa_17_kujeruhiwa
Raia wasiopungua 12 wameuawa na wengine 17 kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika jimbo la Darfur Kaskazini.
(last modified 2025-10-09T07:14:20+00:00 )
Oct 09, 2025 07:14 UTC
  •  Wanamgambo wa RSF washambulia hospitali jimboni Darfur; watu 12 wameuawa, 17 kujeruhiwa

Raia wasiopungua 12 wameuawa na wengine 17 kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika jimbo la Darfur Kaskazini.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa daktari mwanamke na muuguzi mmoja ni miongoni mwa raia waliojeruhiwa katika shambulio hilo la RFS katika hospitali ya El Fasher. 

Kundi hilo la madaktari limelaani shambulio hilo la wanamgambo wa RSF na kulitaja kuwa jinai kamili ya kivita ambayo imepuuza kabisa maisha ya raia na sheria za kimataifa zinazolinda vituo vya afya na wafanyakazi wake.  

Mtandao wa Madaktari wa Sudan aidha umeitaka jamii ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kusitisha mashambulizi katika vituo vya afya na makazi ya raia na kutoa ulinzi kwa mfumo wa afya ulioharibiwa pakubwa katika mji wa El Fasher. 

Wanagambo wa RSF wanaopigana na jeshi la Sudan wameuzingira mji wa El Fasher tangu Mei 10 mwaka jana licha ya tahadhari za kimataifa kuhusu hatari wanazosababisha kwa mji huo ambao ni kitovu cha oparesheni za kibinadamu katika mikoa mitano ya jimbo la Darfur.