DRC yatangaza mripuko wa 16 wa Ebola; WHO yatoa indhari
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza mripuko mpya wa Ebola katika jimbo la kati la Kasai, ambalo ni la 16 nchini humo tangu 1976, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likitahadharisha kuwa huenda maambukizi ya maradhi hayo yakaongezeka.
Waziri wa Afya wa DRC, Roger Kamba alitangaza katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kinshasa jana Alkhamisi kwamba, aina ya virusi vya Ebola ya Zaire imeibuka tena katika eneo la Bulape, ambapo kesi 28 zinazoshukiwa na ugonjwa huo zimeripotiwa, ikiwa ni pamoja na vifo 15. Wafanyakazi 4 wa afya ni miongoni mwa waathiriwa.
"Takwimu hizi bado ni za muda, kwani uchunguzi bado unaendelea," Kamba alisema, akisisitiza kuwa tangazo hilo limetolewa kwa njia ya uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kisayansi.
Sampuli zilizozofanyiwa vipimo Septemba 3 katika Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Tiba ya Kibiolojia ya DRC zilithibitisha chanzo cha mripuko huo kama spishi ya Zaire, Ofisi ya Kanda ya Afrika ya WHO ilisema katika taarifa yake. "Idadi ya kesi huenda ikaongezeka kadri ueneaji unavyoendelea kuripitiwa," imeonya.
"Nchi hii ina akiba ya matibabu, pamoja na dozi 2,000 za chanjo ya Ervebo Ebola, yenye ufanisi wa kujikinga na aina hii ya Ebola, ambayo tayari imetolewa mjini Kinshasa na ambayo itahamishiwa haraka Kasai ili kuchanja waliotagusana na wahudumu wa afya walio mstari wa mbele," WHO imebainisha na kuongeza kuwa, inasambaza tani mbili za vifaatiba, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujikinga, na maabara tamba.
Ikumbukwe kuwa, Septemba mwaka 2022, DRC ilitangaza habari ya kutokomezwa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi. Hadi sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa na miripuko 16 ya Ebola tangu mwaka 1976, ambapo kati ya hiyo, saba imekumba nchi hiyo tangu mwaka 2018. Ebola ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusababisha kifo na hupata binadamu na nyani. Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.