Waasi wa RSF washambulia maeneo muhimu ya kijeshi Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130810-waasi_wa_rsf_washambulia_maeneo_muhimu_ya_kijeshi_sudan
Afisa mmoja wa jeshi la Sudan ameziambia duru za habari kwamba droni kadhaa za wanamgambo wa RSF zimeshambulia vituo muhimu vya kijeshi na miundo mbinu ya raia nchini Sudan.
(last modified 2025-09-15T04:01:35+00:00 )
Sep 15, 2025 04:01 UTC
  • Waasi wa RSF washambulia maeneo muhimu ya kijeshi Sudan

Afisa mmoja wa jeshi la Sudan ameziambia duru za habari kwamba droni kadhaa za wanamgambo wa RSF zimeshambulia vituo muhimu vya kijeshi na miundo mbinu ya raia nchini Sudan.

Afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema mashambulizi hayo yalilenga makao makuu ya jeshi la Sudan pamoja na maghala ya mafuta Magharibi mwa Mto Nile.

Mashambulizi mengine pia yalilenga kambi ya jeshi la anga la Kenana na uwanja mdogo wa ndege Kusini Mashariki mwa mji wa Kosti. Kituo cha umeme cha Um Dubakir pia kilishambuliwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Serikali ya Sudan imetangaza masharti ya msingi kwa ajili ya kukubali juhudi za kimataifa za kusitisha mgogoro unaoendelea nchini humo, ikisisitiza kuwa mpango wowote lazima uheshimu mamlaka kamili ya taifa na uhalali wa taasisi zake za kiserikali.

Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya kundi la nchi nne, linalojumuisha Marekani, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Misri, kutangaza pendekezo la kusitisha mapigano kwa muda wa miezi mitatu kwa sababu za kibinadamu, kabla ya kusitisha mapigano kwa kudumu na kuanza mchakato wa kisiasa wa miezi tisa wa kuunda serikali mpya.

Mapigano yalizuka nchini Sudan mwezi Aprili mwaka 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kwa ajili ya kuwania madaraka; na hadi sasa yamepelekea kuuawa watu zaidi ya 20,000 na kujeruhi wengine wengi. Wasudani wasiopungua milioni 14 pia wamekuwa wakimbizi kufuatia mapigano hayo.