Wananchi wa Malawi wanapiga kura leo, uchumi wazidi kuzorota
Wananchi wa Malawi wanaelekea kwenye vituo vya kupigia kura leo Jumanne katika uchaguzi utakaomchuanisha Rais Lazarus Chakwera na mtangulizi wake Peter Mutharika, huku mfumuko wa bei uliokithiri na uhaba wa mafuta ukizidi kuongeza hasira za wananchi na kuleta uwezekano wa kutoshiriki kwa wingi wananchi kwenye uchaguzi huo.
Wagombea wengine 15 akiwemo rais wa zamani Joyce Banda pia wanawania kiti cha urais, lakini wachambuzi wa mambo wametabiri kwamba mchuano mkali utakuwa baina ya Chakwera, 70, na Mutharika, 85. Kama hatopatikana mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, uchaguzi huo utaingia kwenye duru ya pili.
Malawi imekumbwa na mdororo wa kiuchumi tangu kiongozi wa kanisa, mchungaji Chakwera alipochaguliwa kuwa rais, mwaka 2020, huku kukiwa na kimbunga kikali na ukame ulioangamiza mazao na kupelekea hali ya maisha kuwa mbaya zaidi. Mfumuko wa bei umeongezeka kwa zaidi ya 20% tangu miaka mitatu iliyopita.
Kashfa za ufisadi zimechangia kukatishwa tamaa wananchi. Mchungaji Chakwera aliingia madarakani akiishutumu serikali ya zamani ya Mutharika kwa ufisadi uliokithiri, lakini hali imezidi kuwa mbaya alipoingia madarakani.
Malawi ni nchi yenye takriban watu milioni 22. Katika uchaguzi wa leo Jumanne, wananchi watawapigia kura pia wabunge na madiwani wa serikali za mitaa.
Kuna uwezekano mkubwa kwa chama chochote kitakachoshinda kati ya hivyo viwili vikubwa, kile cha mchungaji Chakwera cha Malawi Congress au cha Mutharika cha Democratic Progressive Party kitalazimika kuunda muungano na vyama vidogo ili kupata viti vingi bungeni.