Kampeni za uchaguzi mkuu wa Uganda wa Januari 2026 zaanza rasmi
Kampeni za uchaguzi mkuu wa Uganda zimeanza rasmi leo Jumatatu kabla ya uchaguzi huo wa Januari 206 ambao huenda ukawa mpambano kati ya Rais aliyeko madarakani Yoweri Kaguta Museveni na mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi Ssentamu, almaarufu Bobi Wine, ukitazamwa kama marudio ya uchaguzi wa 2021.
Tume ya Uchaguzi ya Uganda EC imetoa ratiba rasmi ya kampeni kwa wagombea wote wanane wa urais iliowapitisha kuandaa mikutano yao kote nchini huku wakiepuka mizozo na migongano ya maeneo ya kufanyia kampeni zao.
Wiki iliyopita, tume hiyo iliwaidhinisha Rais Museveni na Bobi Wine kushiriki kinyang'anyiro hicho.
Akiwa na umri wa miaka 81, Museveni anawania kuchaguliwa tena akibeba bendera ya chama tawala cha National Resistance Movement, NRM baada ya kuweko mdarakani kwa karibu miaka 40.
Mwaka 2017, Bunge la Uganda liliondoa ukomo wa umri wa kikatiba wa kuwania urais, na hivyo kutoa mwanya kwa Museveni kugombea kwa muda wowote anaotaka.
Katika mkutano aliofanya na wanahabari wiki iliyopita, kiongozi huyo aliangazia mafanikio yake na kuahidi kuwekeza katika elimu, miundombinu na afya.
Lakini wakosoaji wamelaani ukiukwaji wa haki za binadamu wa serikali yake na namna inavyowakandamiza wapinzani wa kisiasa.
Mshindani wake mkuu Bobi Wine amejenga matumaini ya mabadiliko nchini humo. Mwimbaji huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita wa urais mnamo 2021, kwa kupata 35% ya kura
Wine alidai ushindi wake uliibwa kupitia ujazo wa kura na makosa mengine. Hata hivyo tume ya uchaguzi wa Uganda ilikanusha madai hayo.../