Waandamanaji wa Afrika Kusini wataka Israel iwaachilie wanaharakati wa msafara wa Gaza
Waandamanaji waliokusanyika nje ya ubalozi wa utawala wa Israel nchini Afrika Kusini siku ya Ijumaa wametoa wito wa kuachiliwa kwa wanaharakati raia wa Afrika Kusini na wengine wote waliotekwa nyara na majeshi ya Israel wakiwa katika msafara wa meli unaojulikana kama Sumud uliokuwa ukielekea Gaza kupelekea misaada ya kibinadamu.
Katika jiji la Pretoria, waandamanaji wakiwa na mabango na bendera za kuunga mkono Palestina wameitaka serikali ya Afrika Kusini kufunga ubalozi wa Israel na kumfukuza balozi wake nchini humo.
Waandamanaji hao wamesisitiza kuwa Israel inatekeleza uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Maandamano zaidi yanatarajiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini, taifa linalojulikana kwa msimamo wake wa kuunga mkono Palestina na ambalo limeishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), likiituhumu kwa kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini siku ya Alkhamisi alitaka kuachiliwa mara moja kwa Waafrika Kusini na raia wengine wa kigeni wanaozuiliwa na jeshi la Israel, baada ya wanajeshi wa majini wa utawala huo haramu kushambulia msafara wa kibinadamu uliokuwa unaelekea Gaza.
Ramaphosa amelaani shambulio hilo katika maji ya kimataifa, akisema linaonyesha kuendelea kwa Israel kupuuza sheria za kimataifa sanjari na kushtadi mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo la Palestina linalozingirwa.
"Kuzuiliwa kwa msafara wa kimataifa wa Sumud ni kosa jingine kubwa la Israel dhidi mshikamano wa kimataifa na hisia ambazo zinalenga kupunguza mateso huko Gaza, na kuendeleza amani katika eneo hilo," amesema Ramaphosa katika taarifa.
Rais huyo wa Afrika Kusini ameitaka Israel kuwaachilia huru mara moja raia waliokamatwa na askari wa Israel wakati wa uvamizi huo, na kuruhusu meli za misaada kupeleka mizigo yao kwa wakazi wa Gaza.
"Kwa niaba ya serikali na taifa letu, natoa wito kwa Israel kuwaachilia mara moja Waafrika Kusini waliotekwa nyara katika maji ya kimataifa, na kuwaachilia pia raia wengine ambao walikuwa wanajaribu kufika Gaza kupeleka msaada wa kibinadamu," amesema Ramaphosa.
Amesema kuwa, hatua za Israel zimekiuka uhuru wa nchi ambazo bendera zao zilipeperushwa kwenye meli za msafara wa Sumud na kukiuka amri ya Mahakama ya Kimataifa inayotaka kufikishwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo huko Gaza.
Amesema dhamira ya msafara wa Sumud ilikuwa njia moja ya kutangaza "mshikamano," na wala sio makabiliano, na ameonyesha matumaini kwamba Israel itawaachilia huru haraka wanaharakati iliowateka, akiwemo mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela.