Mwanasiasa mkongwe Raila Odinga aombolezwa; Rais Ruto atangaza siku saba za maombolezo
Rais William Ruto ametangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku saba kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amollo Odinga.
Katika kipindi hiki, bendera zote za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya heshima na maombolezo.
Aidha, Rais Ruto ametangaza kusitisha shughuli zake zote za umma na kuwasihi maafisa wengine wa serikali kuchukua hatua kama hiyo ili kutoa nafasi ya kutafakari na kuomboleza maisha ya kiongozi huyo mashuhuri.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa wa upinzani Kenya, na Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri hiyo, Raila Amolo Odinga.
Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuma rambi rambi zake kwa familia ya Raila Odinga na kuusema: ‘Nimepoteza rafiki na kaka. Kwangu mimi, Raila alikuwa zaidi ya mwenzangu wa kisiasa, alikuwa sehemu ya pekee ya safari yangu, katika utumishi wa umma na maishani’.
Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha mwanasiasa wa Kenya, Raila Odinga na "nasikitisha kusikia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya RailaOdinga.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga.
Na kumtaja Raila Odinga kama kiongozi mashuhuri na rafiki wa dhati wa India.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan naye ametuma salamu za rambi rambi baada ya kifo cha mwanasiasa wa upinzani nchini Kenya, bwana Raila Odinga.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Mama Samia amesema, "nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Tumempoteza kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote."
Kadhalika Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Kenya kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Raila Amolo Odinga.
Katika ujumbe wake, Rais Tinubu amesema anaungana na Wakenya wote katika huzuni kubwa kufuatia kuondokewa na kiongozi ambaye alikuwa na nafasi ya kipekee si tu katika historia ya Kenya, bali pia barani Afrika.